Manchester United wapepesuka

*Man City wawaharibia Wigan
*Chelsea warudi nafasi ya tatu

Ligi Kuu ya England imeendelea kunoga, baada ya mechi tatu za katikati ya wiki, ambapo Manchester United nusura waadhiriwe na West Ham United.
Mashetani Wekundu hawakucheza vizuri, na walikuwa nyuma kwa mabao 2-1 hadi Robin van Persie aliposawazishaa kwa utata.
Raia huyo wa Uholanzi aliaminika alikuwa ameotea, alipotokea mpira wa Shinji Kagawa uliogonga milingoti yote ya goli katika kipindi cha pili, RVP akionekana dhahiri kuwa amejenga kibanda.
Hata hivyo, bao hilo lilikubaliwa na kuwafanya United kuambulia pointi moja kwa West Ham wanaofundishwa na Sam Allerdyce, ambao watahamia kwenye Uwanja wa Olimpiki ukishafanyiwa marekebisho.
Manchester City nao walibidi kufanya kazi ya ziada kuweza kuwashinda wagumu Wigan, na ilikuwa kwa bao la kipindi cha pili la Carlos Tevez, kwani suluhu ilikuwa inanukia Etihad.
Kama si uhodari wa golikipa wa kimataifa wa England, Joe Hart, City wangeweza kutunguliwa, kwani mshambuliaji Franco Di Santo hakuwa na ajizi katika kipindi cha kwanza.
Ushindi huo ukichanganywa na sare ya United, bado unatoa nafasi, japo finyu, kwa vijana wa Roberto Mancini kutetea ubingwa wao, iwapo United watafungwa katika baadhi ya mechi walizobakisha.
Kwa upande mwingine, Wigan wamebaki katika timu tatu za kushuka daraja, na wanahitaji pointi tatu kujinasua humo, jambo ambalo wamekuwa wakifanya mwishoni mwa msimu katika miaka ya karibuni.
Chelsea waliovuliwa ubingwa wa Kombe la FA hivi karibuni, wamerejea kishindo kwenye ligi, kwa kuwakandika Fulham mabao 3-0, moja likifungwa na beki Mbrazili David Luiz na mawili nahodha John Terry.
Ushindi huo umewarejesha Chelsea nafasi ya tatu, wakiwavuka Arsenal kwa pointi moja, na bado wana mchezo mmoja mkononi. Arsenal wanafuatiwa na Tottenham Hotspurs kwa tofauti ya pointi mbili, na Spurs pia wana mchezo mmoja mkononi.

Comments