Real Madrid wawanyonga Galatasaray

*Akina Drogba wachoka mapema

Real Madrid wametumia vyema uwanja wa nyumbani kwa kuwafunga Galatasaray na kuwanyima bao la ugenini.
Katika mchezo ulioanza kwa nguvu na ushindani kwa pande zote mbili, Real wanafundishwa na Jose Mourinho ‘The Only One’ walijiamini na kuwazidi nguvu wageni.
Ushindi wao wa mabao 3-0 ni msingi tosha watakapoenda kurudiana na timu hiyo ya Uturuki yenye nyota kama Didier Drogba, Weysley Sneider na Emmanuel Eboue.
Cristiano Ronaldo alifungua kitabu cha mabao dakika ya tisa, akaungwa mkono na Karim Benzema dakika ya 29 na Gonzalo Higuain dakika ya 73.
Drogba, Eboue na wenzao walijitahidi kushambulia na kulenga goli, lakini kadiri muda ulivyokwenda walidhihirisha kuchoka, kisha kuparaganyika mfumo wa uchezaji, wakabaki kutafutana uwanjani.
Mourinho baada ya mechi alipoulizwa mrejesho wake kuhusu aina ya mchezo walioonesha wachezaji wake, alisema wamekuwa makini dimbani.
Real Madrid wanawania kutawazwa mabingwa wa Ulaya kwa mara ya 10. Hata hivyo, hawajatwaa kombe hilo tangu 2002 kwa bao la aina yake Zinedine Zidane alilowafunga Bayer Leverkusen.
Katika robo fainali nyingine, Malaga wa Hispania walitoshana nguvu bila kufungana na Borussia Dortmund nchini Hispania.
Mechi za marudiano zitafanyika wiki ijayo jijini Istanbul kati ya Real na Galatasaray wakati ile ya Malaga na Borussia Dortmund itapigwa Dortmund kuamua timu mbili zitakazoingia nusu fainali.

Comments