Wanariadha wa Kenya wafungiwa kwa madawa

Wakenya wawili wanaoshiriki mbio za marathon wamefungiwa baada ya kutiwa hatiani kwa kutumia dawa za kuongeza nguvu michezoni.

Hatua hiyo inakuja baada ya wanariadha wengine watatu wa nchi hiyo kusimamishwa mwezi uliopita.

Katibu Mkuu wa Chama cha Riadha cha Kenya, David Okeyo amewataja waliofungiwa kwa miaka miwili ni Salome Jerono Biwott na Jynocel Basweti Onyancha.

Mwezi uliopita, wakimbiaji wa mbio ndefu, Wilson Erupe Loyanae na Nixon Kiplagat Cherutich walifungiwa kwa miaka miwili wakatiMoses Kiptoo Kurgat alipewa kifungo cha mwaka mmoja.

Wiki iliyopita, mwanahabari wa kujitegemea wa Ujerumani, Hajo Seppelt alibainisha matokeo ya uchunguzi kwamba kuna tatizo kubwa la utumiaji dawa za kuongeza nguvu kwa wanariadha nchini Kenya.

Taarifa hiyo ilitolewa kabla ya kufanyika Michuano ya 30 ya Olimpiki jijini London mwaka jana. Kenya na Ethiopia zimekuwa zikitawala kwenye mbio ndefu

“Idadi ya watumiaji dawa hizi inaongezeka na kwa kweli tumeudhika sana na takwimu na hali hii kwa ujumla.

“Tunachoomba tu ni kwamba wakosaji hao wawe katika ngazi inayoweza kudhibitiwa, isije ikatokea tatizo limesambaa kutuzidi nguvu,” akasema Okeyo.

Katika michuano hiyo ya Olimpiki, Kenya iitwaa jumla ya medali 11, mbili zikiwa za dhahabu, nne za fedha na tano za shaba, lakini zinagawanywa katika michezo mbalimbali, ikiwamo riadha.

Comments