SUALA LA AKINA MORRIS, CANNAVARO KWENDA KAMATI YA NIDHAMU

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepokea barua ya Chama cha
Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFA) ikieleza kuwafungia wachezaji kadhaa
Wazanzibari wanaochezea klabu mbalimbali za timu za Tanzania Bara na timu
ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars).

Suala hilo limepelekwa kwa Kamati ya Nidhamu na Usuluhishi ya TFF kwa hatua
zaidi, hivyo kwa sasa Shirikisho litasubiri uamuzi wa kamati hiyo. Baadhi
ya wachezaji hao ni nahodha msaidizi wa Taifa Stars, Aggrey Morris, Nadir
Haroub ‘Cannavaro’, Nassoro Masoud Cholo, Mcha Khamis, Seif Abdallah na
Selemani Kassim Selembe.

*MTIBWA YAINGIA NUSU FAINALI KOMBE LA UHAI*

Mtibwa Sugar imekata tiketi ya kucheza nusu fainali ya michuano ya Kombe la
Uhai inayoshirikisha timu za vijana wenye umri chini ya miaka 20 za klabu
za Ligi Kuu ya Vodacom baada ya leo asubuhi (Desemba 19 mwaka huu)
kuzamisha African Lyon mabao 3-1.

Katika mchezo huo uliofanyika Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Dar es Salaam,
hadi mapumziko Mtibwa Sugar ilikuwa mbele kwa bao 1-0 lililofungwa dakika
ya 22 na Hillary Kasela. Hassan Kabunda aliisawazishia African Lyon katika
dakika ya 53.

Mabao mengine ya washindi yalifungwa na Godfrey Mohamed dakika ya 64 na
Juma Lazio akapachika la mwisho dakika ya 87. Kwa ushindi huo, Mtibwa Sugar
sasa itacheza mechi ya kwanza ya nusu fainali dhidi ya Azam ambayo nayo leo
asubuhi (Desemba 19 mwaka huu) iliilaza JKT Ruvu bao 1-0 katika mchezo
uliofanyika Uwanja wa Chamazi. Bao la Azam lilifungwa dakika ya 46 na
Mudathiri Yahya.

Mechi hiyo ya kwanza ya nusu fainali itachezwa Ijumaa (Desemba 21 mwaka
huu) saa 8 kamili mchana kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Dar es
Salaam. Nusu fainali ya pili nayo itachezwa kwenye uwanja huo huo kuanzia
saa 10 kamili jioni.

Robo fainali ya tatu kati ya Oljoro JKT na Simba, na robo fainali ya nne
zinachezwa leo saa 10 kamili jioni (Desemba 19 mwaka huu) kwenye viwanja
vya Karume na Chamazi, Dar es Salaam.

Mechi ya fainali na ile ya kutafuta mshindi wa tatu zitachezwa Jumapili
(Desemba 23 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Dar es Salaam.

Comments