TOC kukutana Zanzibar kujadili mkutano

Wakati fomu za kuwania uongozi wa TOC zemeanza kutolewa, kamati ya utendaji ya kamati hiyo ya Olimpiki inatarajia kukutana Novemba 17 visiwani Zanzibar kwa ajili ya kujadili matayarisho ya mkutano mkuu na uchaguzi.

Akizungumza na NIPASHE jana, katibu mkuu TOC, Filbert Bayi alisema mkutano mkuu umepangwa kufanyika Desemba 6 mkoani Dodoma.

Aidha alisema katika kikao cha kamati ya utendaji ya TOC, watajadili kuhusiana na uchaguzi mkuu wa viongozi, pamoja na matayarisho ya mkutano mkuu ambao utatangulia kabla ya uchaguzi mkuu.

Bayi alisema katika kikao hicho, TOC watapanga jinsi vyama vitakavyotoa mwakilishi mmoja kwa ajili ya kupiga kura, pamoja na kutoa maelekezo nini vyama vinatakiwa kufanya ili viweze kushiriki katika uchaguzi huo.

Alisema fomu kwa ajili ya kuwania nafasi za uongozi tayari zimeanza kutolewa katika ofisi za kamati hiyo.

Alizitaja nafasi zinazowaniwa katika kinyang’anyiro hicho ni pamoja na Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti, Katibu Mkuu, Katibu msaidizi, Mweka Hazina na msaidizi wake, pamoja na wajumbe kutoka Bara na Visiwani.

Alisema usaili umepangwa kufanyika Novemba 20 jijini Dar es Salaam, na Novemba 24 utafanyika visiwani Zanzibar.

Mbali na hilo kabla ya uchaguzi mkuu wa TOC, kutakuwa na uchaguzi wa kamisheni ya wachezaji (KAWATA) ambao nao utafanyika Desemba 6 mkoani Dodoma.

Viongozi watakaochaguliwa katika uchaguzi huo watakaa madarakani kwa muda wa miaka minne kwa mujibu wa katiba

Comments