Salaam za Olimpiki …Na Gloria Mutahanamilwa

Nakumbuka wakati London inapewa nafasi ya kuandaa Michezo ya Olimpiki 2012, niliona ni mbali mno.

Tangu kipindi hicho kumekuwa na maandalizi ya viwanja na wachezaji pia hadi uchochoroni ambapo hadi watoto chini ya miaka 10 walionekana wakijifua kwa ajili ya Olimpiki ya miaka saba ijayo.

Na kweli baadhi yao wamekuwa wakubwa, wakapata viwango, kushiriki na hata kujinyakulia medali za Olimpiki.

 

Mwakilishi wetu wa kuogelea, hakuchelewa sana kimaandalizi manake alijiunga na timu wiki moja kabla ya safari ingawa wenzake walianza kukusanywa mwezi mmoja kabla.

Wakawekwa kambini pale maeneo ya Kibaha, Kibaha inayotajwa mara kwa mara zitokeapo ajali za barabarani Tanzania Bara.

Sina uhakika ni mara ngapi vyombo vya habari vimefuatilia kuhusu maandalizi ya Tanzania kwa Olimpiki japo katika kipindi hicho cha mwezi mmoja.

Sijaona hayo makampuni ya simu wala taasisi za benki zikifanya promosheni ya futari kwa wanamichezo wetu kabla ya safari ya Olimpiki.

Sina uhakika ni kwa kiasi gani wadau wakuu wa michezo yaani Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, walijitolea kabla ya safari iliyofikia tamati Jumapili.

Lakini ingepatikana medali, mbona kila mmoja wetu angetaka aonekane yeye kwa hotuba za pongezi na shukrani kwa mamlaka husika.

Kwani nini bwana, mbona Tanzania madini ya kumwaga, si tuongee na wawekezaji tu watutengenezee vijiduara vya dhahabu wawakilishi wetu nao watinge mjengoni Dodoma!

Nionavyo mimi, sasa hivi mazoezi yawe ya kutunisha misuli tu kwenye Olimpiki ya 2016 itakayofanyika Rio de Janeiro, Brazil.

Hapo angalau wawakilishi wetu wa kike wajitande khanga na wanaume wakivaa kanzu na bakora si mbaya ili kamera zitumulike wakati wa sherehe za ufunguzi.

Na mwakani tutakapojua michezo ya Olimpiki ya 2020 itafanyikia wapi, basi tuwasaidie viongozi wa vyama vya ridhaa vya michezo kifedha na hata kiintelinjisia pia.

Posted under:  Olympics sports, Sports News

Tags:  

Comments