Yanga yapoteza rufani…..

Matumaini ya Yanga kutetea ubingwa wao wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara yalipata pigo la kubwa jana wakati Kamati ya Nidhamu ya shirikisho la soka nchini (TFF) ilipotupilia mbali rufaa yao ya kupinga kukatwa pointi 3 walizopata katika mechi dhidi ya Coastal Union baada kumchezesha beki wao Nadir Haroub ‘Cannavaro’ ambaye alipaswa kutumikia adhabu ya kutocheza mechi tatu kutokana na kadi nyekundu aliyopewa katika mechi yao Machi 10 dhidi ya Azam FC lakini akatumikia mechi mbili.

Kwa mujibu wa taarifa za ndani kutoka katika kikao cha Kamati ya Nidhamu kilicho chini ya mwenyekiti wake Alfred Tibaigana kilichomalizika takriban saa 4 usiku jana, Yanga hawakuwa na hoja za msingi katika rufaa yao na kwamba maamuzi ya mechi ya dhidi ya Azam yalikuwa sahihi.

Kwa maana hiyo, Coastal Union itabaki na pointi tatu na magoli matatu waliyopewa na Kamati ya Ligi kufuatia kosa la Yanga kumchezesha beki huyo wa kati.

Hata hivyo, Yanga bado wanayo nafasi ya kukata rufaa katika ngazi ya juu zaidi ambayo ni Kamati ya Rufaa ya TFF, taarifa hiyo ilisema.

Yanga walikatwa pointi tatu baada ya kushinda 1-0 dhidi ya Coastal Union mkoani Tanga kupitia kwa goli la Hamis Kiiza lakini adhabu hiyo inamaanisha kwamba timu hiyo ya Jangwani itabaki na ponti 43, kumi nyuma ya vinara na mahasimu wao Simba huku zikiwa zimebaki mechi 3 ligi kumalizika.

Yanga imebakisha mechi nne. Azam ni ya pili katika msimamo ikiwa na pointi 50.

Posted under:  All Articles

Tags:  

Comments