Wanariadha 5,000 kushiriki `Kilimanjaro Marathon 2012`

Wanariadha zaidi ya 5,000 kutoka katika nchi 40 watashiriki katika mashindano maarufu ya riadha yanayotimiza miaka kumi tangu kaunzishwa kwake ya ‘Kilimanjaro Marathon 2012’.

Waandaaji wa mashindano hayo walisema jijini Dar es Salaam jana kuwa mbio za mwaka huu zitafanyika Feburuari 26 na kuwahusisha wanariadha wanaotoka katika mabara sita.

Imeelezwa kuwa wahsiriki watashindana katika sehemu nne za mbio hizo, ambazo ni mbio za Kilimanjaro Premium Lager (Kilimanjaro Premium Lager Marathon), mbio za nusu marathon, mbio fupi za GAPCO zinazowahusisha walemavu (GAPCO Disabled Half Marathon) na mbio za Kilometa Tano za Vodacom (Vodacom 5 km Fun Run).

Kampuni ya Wild Frontiers ya Afrika Kusini ndio inayoaandaa Mbio za Kilimanjaro ambazo huratibiwa na kampuni ya Kitanzania ya Executive Solutions, kwa kushirikiana na Chama cha Riadha taifa na cha mkoa wa Kilimanjaro.

“Tunatarajia kuwa na wanariadha kutoka katika nchi 40 watakaotoka katika mabara sita tofauti,” alisema John Addison, mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya Wild Frontiers.

Mbali na wanariadha kutoka Tanzania, baadhi ya nchi ambazo washiriki wanatarajiwa kutoka ni Uganda, Burundi, Rwanda, Kenya, Msumbiji na Zambia. Nyingine ni Malawi, Zimbabwe, Ethiopia, Afrika Kusini, Marekani, Japan, Italy, Canada, Ufaransa, Ujerumani, Sweden, Norway na Australia.

Wakati zilipoanza mwaka 2003, mbio za Kilimanjaro Marathon ziliwahusisha wanariadha 750 tu, wengi wao wakitoka katika nchi za Tanzania, Kenya, Ethiopia, Uganda, Zimbabwe na Afrika Kusini. Katika mbio za mwaka jana. washiriki 4,500 kutoka katika nchi 35 walijitokeza.

George Kavishe, Meneja wa bia ya Kilimanjaro Premium Lager ambao ndio wadhamini wakuu wa mbio hizo, alikumbushia kuwa mwanariadha Lucian Hombo wa Tanzania alipata ushindi wake wa kwanza katika mbio za Kilimanjaro kwa muda wa 2:16:25 na baada ya hapo, amekuwa nyota na kushinda katika mashindano mbalimbali yanayoandaliwa katika nchi tofauti duniani.

Aliwataja wanariadha wengine waliowahi kuibukia katika mbio za Kilimanjaro na hadi sasa wameendelea kufanya vizuri kuwa ni pamoja na Christopher Isegwe na Banuelia Brighton.

Mbali na Kilimanjaro Premium Lager, wadhamini wengine ni  Maji ya Kilimanjaro, Vodacom, Gapco Tanzania, CFAO Motors, Keys Hotels, KK Security, Simba Cement, Tanzanite One, TPC Sugar, Precisionair, Southern Sun na Bodi ya Utalii Tanzania.

Posted under:  All Articles

Tags:  

Comments