Azam yawawashia taa Yanga na Simba…..

HATIMAYE , timu ya soka ya Azam FC, imewasha taa ya kujizolea mashabiki wa mchezo huo Tanzania kwa kuzitangazia umwamba timu kongwe za Simba na Yanga katika Michuano ya Kombe la Mapinduzi ya Zanzibar inayofanyika uwanja wa Amani.

Timu hiyo imefanikiwa kuingia kwenye fainali na kuweka hai ahadi ya kulitwaa kombe hiyo baada ya kuwatimua Simba kwenye nusu fainali kwa mabao 2-0 wakati wa mechi iliyochezwa usiku wa kuamkia Januari 10.

Kipigo hicho kwa simba kiilitokea siku chache baada ya watani wao wa jadi Yanga yenye mashabiki wengi Tanzania nayo kupokea kichapo cha magoli 3-0 katika mechi ya raudi ya robo fainali kutoka kwa Azam.

Kwa hali hiyo, Azam imefanikiwa kuzitimua timu hiyo huko Zanzibar  huku ikibaki  kwenye fainali na timu nyingine ya Zanzibar ambayo itapatikana usiku wa kuamkia Januari 11 katika mechi itakayoshirikisha timu za Jamhuri na Mafunzo.

Tayari Yanga iluishatangaza kwamba Azam sasa ni timu pinzani kali kama Simba baada ya kukubali vipigo viwili tofauti kwani mwishoni mwa mwaka jana ilifungwa magoli 2-0 na mwaka huu kukubali magoli 3-0 kutoka kwa timu hiyohiyo.

Baadhi ya mashabiki wa soka Dar es Salaam wameelezea vipigo hivyo kwa timu za Simba na Yanga kuwa ni mwanzo wa kupoteza umaarufu  huku wengine wakisema watahamia ushabiki wao Azam.

Timu ya Azam ilianzishwa miaka michache iliyopita na mfanyabiashara maarufu  nchini na kuweza kujenga uwanja wa kisasa ukiwa na vyumba mbalimbali vya mazoezi na starehe.

Lakini pia  uongozi wa timu hiyo umeajiri kocha kutoka uingereza na kupewa jukumu la kuiunda timu imara itakaoleta ushindani Afrika.

Kwenye ligi kuu Tanzania inashika nafasi ya tatu ikiwa chini ya Yanga  na Simba, lakini kwa kasi iliyonayo sasa kama itaingia nayo kwenye mzunguko wa pili wa ligi hiyo, upo uwezekano  ikatwaa ubingwa.

Posted under:  All Articles

Tags:  

Comments