Timu kongwe zadhalilishwa zanzibar

Miamba ya soka Tanzania,Simba na Yanga zimedhalilika mjini Zanzibar zinakoshiriki michuano ya kuwania kombe la Mapinduzi  inayofanyika Uwanja wa Amani  mjini humo.
Yanga ndiyo iliyoonja joto kali la jiwe baada ya kujikuta ikichapwa tena magoli 3-0 na timu ya walamba koni ya Azam FC  katika mechi  ambayo ilikuwa ya kutafutwa mshindi wa pili atakayeingia kwenye raundi ya nusu fainali kwenye kundi lake.

Awali Yanga ilifungwa goli 1-0 na timu ya Mafunzo ya Zanzibar na baadaye ilifanikiwa kuichabanga timu ya Kikwajuni magoli 2-0  kabla ya kuaga michuano hiyo kwa kukubali magoli 3-0 dhidi ya Azam.

Katika kundi hilo, timu ya Azam na Mafunzo ndizo zilizofanikiwa kuingia nusu fainali kuwania kombe hilo la uhuru kwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

Nayo Simba ilianza michuano hiyo kwa kutandikwa magoli 3-2 na timu ya Jamhuri kutoka Pemba , lakini baadaye ikafufua matumaini baada ya kuichapa timu ya Miembeni magoli 4-3 katika mchezo ambao wengi walisema timu hiyo ililemewa.

Baadhi ya mashabiki walisema Simba iliokolewa na kiongozi wa timu ya Miembeni akidaiwa kwamba alikwenda kwenye benchi la ufundi dakika za mwisho na kutoa maelekezo ambayo yanadaiwa ya kuwapoza wachezaji watoe mwanya kwa SDimba kushinda.

Hata hivyo uvumi huo ulipingwa vikali na viongozi wa Simba ambao walisisitiza kwamba  walishinda kihalali.

Pamoja na ushindi huo, Simba ya sasa inaonyesha udhaifu mkubwa katika eneo la ulinzi kwani inakubali kufungwa magoli mengi tofauti na  matarajio ya mashabiki wa timu hiyo.

Simba usiku wa kuamkia leo inatarajia kuchuana na KMKM  na tayari iumeapa kufia uwanjani ili kushinda mechi hiyo.

lakini kwa upande wa vijana wa Zanzibar kwa pamoja wameungana  na kusisitiza kwamba kombe la Mapinduzi mwaka huu lazima libaki Zanzibar.

Posted under:  All Articles

Tags:  

Comments