Simba wadaka`mihela` TBL

Timu ya Simba

Wakati klabu ya ‘Wekundu wa Msimbazi’, Simba ikithibitisha kupokea hundi ya fedha za mishahara ya wachezaji wake jana kutoka kwa wadhamini wao, Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), hali ya kifedha kwa wachezaji wa watani zao wa jadi, Yanga ambao pia hudhaminiwa na kampuni hiyo bado iliendelea kuwa ya utata kwani hadi kufikia jana mchana walikuwa bado hawajalipwa mishahara hiyo, imefahamika.

Afisa Habari wa klabu ya Simba, Ezekiel Kamwaga, aliiambia NIPASHE jana kuwa TBL waliwakabidhi hundi ya fedha za mishahara ya wachezaji wao kama mkataba wa kampuni hiyo na klabu yao na mahasimu wao Yanga unavyoeleza.
“Sisi tunashukuru kwani tumeshakabidhiwa hundi na TBL kwa ajili ya mishahara ya wachezaji na wafanyakazi wa klabu yetu… hata hivyo, wachezaji na wafanyakazi wote wa Simba walishalipwa mishahara yao na hivyo hatukuwa na matatizo yoyote yaliyotokana na fedha hizi kutoka TBL, ,” alisema Kamwaga.
Afisa Habari wa Yanga, Louis Sendeu hakuwa tayari kuthibitisha kama wamepokea hundi kutoka TBL kama wtaani zao Simba, kwa madai kuwa suala hilo ni la ndani ya klabu yao.
“Kama Simba wameamua kutoa taarifa za mishahara yao kwenye vyombo vya habari ni wao, lakini sisi tuna taratibu zetu… hatuwezi kuwaambia kama tumelipwa na TBL au bado kwa sababu huo sio utaratibu wetu,” alisema Sendeu.

Hata hivyo, Sendeu alishakaririwa mara kadhaa akizungumzia suala la mishahara, mojawapo akisema kuwa chanzo cha kuchelewa kulipwa kwa wachezaji wao ni kuchelewa kwa hundi ya fedha hizo kutoka kwa wadhamini wao TBL.  

Wakizungumza na NIPASHE kwa sharti la kutotajwa gazetini, baadhi ya wachezaji wa ‘Wanajangwani’ walisema kwamba hali yao kifedha bado mbaya kwani bado hawajalipwa mishahara. Mmoja wa wachezaji hao alidai kuwa hawajalipwa tangu Novemba.
Kocha wa Yanga, Kostadin Papic alifichua hali mbaya ya kifedha waliyo nayo klabuni kwao na kutahadharisha kuwa asije kulaumiwa mtu pindi timu yake ikifanya vibaya katika mechi zao za mzunguko wa pili wa ligi kuu ya Bara na pia katika mechi yao ya ligi ya Klabu Bingwa Afrika dhidi ya Zamalek ya Misri.

Papic alifichua kuwa wachezaji wake wamepoteza morari kutokana na ukata na kwamba, walishindwa kufanya mazoezi kwa siku saba kwa sababu ya kukosa fedha za kulipia uwanja na hata kwenye gym.

Baada ya kilio cha Papic, timu hiyo hatimaye ilianza mazoezi juzi kwenye Uwanja wa Loyola uliopo Mabibo jijini Dar es Salaam. 

Posted under:  All Articles

Tags:  

Comments