NMB yamwaga vifaa vya m.9/-

Benki ya NMB imetoa vifaa mbalimbali vya michezo kwa timu hiyo kwa ajili ya kujiandaa na mechi yao ya ugenini ya mchujo wa kuwania kufuzu hatua ya awali ya makundi ya Kombe Dunia dhidi ya Chad itakayofanyija Novemba 11 mjini N’Djamena.

Poulsen alisema kuwa amemuita Bocco kikosini kutokana na uwezekano wa kumpata mshambuliaji Danny Mrwanda anayecheza soka la kulipwa nchini Vietnam kuwa mdogo.

Poulsen alisema kuwa kikosi chake kilitarajiwa kuanza mazoezi jana jioni na nyota wanaocheza nje ya Tanzania watawasili nchini kuanzia keshokutwa na hiyo inatokana na kupatiwa ruhusa na klabu zao kulingana na kanuni za Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) zinavyoeleza.

Mapema jana asubuhi, Mkurugenzi wa Masoko wa NMB, Imani Kajura, alilikabidhi Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) vifaa vyenye thamani ya Sh. milioni 9 kwa ajili ya mazoezi na mechi zote mbili dhidi ya Chad ambazo zitafanyika wiki ijayo.

Kajura alisema kwamba NMB inafahamu kwamba Stars inakwenda vitani na ndio maana imewapatia vifaa hivyo vya kujiandaa na mechi hizo mbili na wanaamini kwamba ushindi utapatikana na hatimaye kufuzu kwa hatua ya awali ya makundi ya Kombe la Dunia.

Aliwataka wadau wa michezo waungane kwa nguvu zote kama wanavyokuwa wakati wanapozishabikia klabu zao kwa kuwa ni wajibu wa Watanzania wote kuishangilia Stars.

“Tunawaomba wadau wengine waungane na tumeandaa kauli mbiu isemayo “Wiki ya Uzalendo”, ambayo inahamasisha kukuza ushirikiano na kuwataka mashabiki kujitokeza katika mchezo wa marudiano utakaofanyika hapa nyumbani,” alisema Kajura.

Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah, aliishukuru NMB kwa kuwakabidhi vifaa hivyo na kusema kwamba TFF inafahamu kuwa mechi hiyo ni ngumu na vijana watapambana kufa na kupona ili kupata ushindi.

Osiah aliwaomba wadau wa soka kujitokeza zaidi kuisaidia Stars kwani fedha ambazo hutolewa na wadhamini na nyingine wanazopata kupitia viingilio huwa hazitoshi kuiendesha timu hiyo kwa ufanisi.

Wakati huo huo, jana mchana, wadhamini wakuu wa timu hiyo, Kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL) ilizindua kampeni maalumu ya kuhamasisha mashabiki kuungana katika kuishangilia Stars ili ishinde katika mechi zake zote.

Mwenyekiti wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Dioniz Malinzi, aliyekuwepo katika uzinduzi huo, aliwashukuru SBL kwa kuidhamini Stars na kuyaomba makampuni mengine yajitokeze zaidi kuisaidia timu hiyo.

Stars itaondoka nchini Novemba 9 kuelekea Chad na itarejea nyumbani Novemba 12 kujiandaa na mechi ya marudiano itakayochezwa Novemba 15 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Posted under:  All Articles

Tags:  

Comments