Yanga mabingwa Kagame

Timu ya Yanga ya Tanzania leo hii imekuwa bingwa wa Michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kagame Cup mwaka 2011 baada ya kuifunga timu ya Simba pia ya Tanzania kwa goli 1 – 0 katika mchezo wa fainali wa kukata na shoka uliofanyika katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam Tanzania.

Tangu mwanzo wa mchezo timu zote zilionekana kuwa na kiu ya kupata ushindi lakini Simba ndio walioonekana kujipanga vizuri na kulishambulia lango la Yanga katika kipindi cha kwanza hata hivyo baadae Yanga nao walicharuka na kulisakama lango la Simba.

Hata hivyo washambuliaji wa timu zote mbili hawakuweza kupenya na kuleta madhara.

Hadi dakika 90 za kawaida zinamalizika hakuna timu iliyoweza kuona lango la mwenzake. Hivyo ikalazimu kuongezewa dakika 30 za nyongeza na ndipo katika dakika ya 109 Keneth Asamoah wa Yanga akafanikiwa kupachika goli zuri baada kupata pasi kutoka kwa Rashid Gumbo.
Hadi mwisho wa mchezo baada ya nyongeza ya dakika 30 matokeo yakawa 1 – 0.
Kwa matokeo hayo Yanga ya Tanzania wanakuwa mabingwa wa Kombe CECAFA kwa upande wa vilabu Kagame Cup kwa 2011 na hivyo kuondoka na kitita cha dola za kimarekani 30,000.

Mshindi wa pili ambaye ni timu ya Simba amepata dola 20,000Awali katika mechi ya kutafuta mchindi wa tatu wa mashindano hayo timu ya Al Mereikh ya Sudan iliifunga St. George ya Ethiopia magoli 2 – 0 na hivyo kuwa mshindi wa tatu wa michuano hiyo ambayo nayo imejinyakulia dola 10,000.

Posted under:  All Articles

Tags:  

Comments