Henry Joseph, Kiggi waachwa Stars

Kiungo wa kimataifa, Henry Joseph, anayecheza soka la kulipwa nchini Norway, ameachwa nje ya kikosi cha timu ya taifa, Taifa Stars, kilichotarajiwa kuondoka alfajiri ya leo kwenda Jamhuri ya Afrika ya Kati kwa ajili ya kuwakabili wenyeji katika mechi yao ya nne ya hatua ya makundi ya kuwania kufuzu kwa fainali za Mataifa ya Afrika (CAN) 2012, kutokana na kuumia paja akiwa mazoezini.

Wakati akiwataja wachezaji watakaoambatana na timu hiyo katika safari ya leo, kocha wa Stars, Jan Poulsen, aliwaacha pia Kiggi Makassi, ambaye sasa atajiunga na kambi ya timu ya taifa ya vijana ya U23 itakayocheza Jumapili mechi ya kuwania kufuzu kwa Michezo ya Olimpiki dhidi ya Nigeria kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam, na kiungo, Ramadhan Chombo ‘Redondo’.

Wachezaji waliotarajiwa kuondoka leo kwa ajili ya mechi hiyo itakayochezwa Jumapili saa 10:00 jioni (sawa na saa 11:00 jioni kwa saa za Tanzania), ni Shaban Kado, Shaban Dihile, Shadrack Nsajigwa (nahodha), Idrisa Rajab, Amir Maftaha, Juma Nyosso, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ na Aggrey Morris.

Wengine ni Shaaban Nditi, Jabir Aziz, Nudin Bakar, Nizar Khalifan, Julius Mrope, Mbwana Samata, John Bocco, Mrisho Ngassa, Mwinyi Kazimoto, Salum Machaku, Mohamed Banka na Athuman Machuppa.

Mkuu wa msafara huo alitajwa kuwa ni Samwel Nyala, ambaye ni mjumbe wa kamati ya utendaji ya shirikisho la soka nchini (TFF).

Stars pia imewakosa wachezaji wake wa kimataifa, Danny Mrwanda na Abdi Kassim, ambao klabu yao inayoshika mkia ya Dong Tam Long An ya Vietnam imewazuia kuja kujiunga na timu yao ya taifa kwa madai ya kukabiliwa na mechi ngumu za ligi kuu ya nchini humo wakati wakipigania kuepuka kushuka daraja. Hata hivyo, TFF imeishitaki klabu hiyo kwa shirikisho la soka duniani (FIFA) kutokana na jambo hilo.

Kikosi cha kocha, Mdenmark Jan Poulsen, pia kimemkosa kipa wake, Juma Kaseja, aliyejiondoa kwenye timu hiyo kutokana na kuwa majeruhi baada ya kuumia kwenye mchezo wa klabu yake ya Simba dhidi ya Wydad Casablanca walikotolewa katika mashindano ya Ligi ya Klabu Bingwa nchini Misri wiki iliyopita.

Wakati akiwakabidhi bendera ya taifa kwenye ofisi za TFF jana jioni, Mwenyekiti wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Iddi Kipingu, aliwataka wachezaji wakapigane kiume kuipeleka Tanzania katika michuano ya CAN, jambo ambalo limeshindikana kwa miaka tele.

Katika mechi ya mzunguko wa kwanza ya hatua hiyo ya makundi, Stars iliifunga Afrika ya Kati 2-1 kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam na kufanya Kundi D linalohusisha pia timu za Morocco na Algeria kuwa gumu baada ya kila timu kufikisha pointi 4 baada ya mechi tatu.

Fainali zijazo za Mataifa ya Afrika zitaandaliwa kwa pamoja katika nchi za Gabon na Equartorial Guinea.

Posted under:  All Articles

Tags:  

Comments