Ngassa hauzwi-Azam

Uongozi wa klabu ya Azam inayoshiriki Ligi Kuu ya Tanzania Bara umewataka mabingwa wa soka Tanzania Bara, Yanga wasahau kabisa wazo la kumpata tena winga wao wa zamani, Mrisho Ngassa.

Awali, Yanga ilikana kumuhitaji Ngassa lakini mapema wiki hii ilituma kwa Azam maombi rasmi ya kumsajili winga huyo na bila kuchelewa, Azam wakawajibu juzi kwamba hawako tayari kumtoa mchezaji huyo.

Akizungumza na NIPASHE, Katibu Mkuu wa Azam, Nassor Idrissa, alisema kwamba Ngassa ni mchezaji wanayemuhitaji na endapo Yanga wanamtaka mchezaji wa aina yake, ni bora wakaanza mchakato wa kutafuta wachezaji wengine na si huyo ambaye wao walimpata kwa gharama kubwa kutoka kwao (Yanga) msimu uliomalizika.

Idrissa aliongeza kuwa Azam hawako tayari kumuuza Ngassa kwa Yanga au klabu nyingine yoyote na hivyo wasijisumbue kutuma maombi ya kumsajili.

“Ngassa hauzwi ng’o, hivyo ndivyo tunavyosema Azam… wakatafute wachezaji Ghana au Nigeria, na si Ngassa ambaye tulimsajili kwa gharama kubwa kutoka kwao (Yanga),” alisema Idrissa.

Alisema kwamba Azam ambayo msimu ujao imepania kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Bara, inamuhitaji Ngassa ili watimize malengo yao.

Hata hivyo, alisema kuwa endapo mchezaji huyo ataivutia klabu ya nje ya nchi watakuwa tayari kufanya mazungumzo na kwamba hivi sasa, wanaangalia uwezekano wa kuboresha mkataba wa Ngassa ambaye aliibuka kinara wa kupachika mabao katika msimu uliomalizika hivi karibuni.

Kabla ya kupokea barua ya Yanga, Idrissa aliwahi kusema kwamba wao wako tayari kufanya mazungumzo na timu yoyote itakayowafuata kwa ajili ya mzungumzo.

Afisa Habari wa Yanga, Louis Sendeu, aliiambia NIPASHE kwamba wao bado hawajakata tamaa ya kumnasa Ngassa na wataendelea na mazungumzo ya kumsajili wakati dirisha la usajili litakapofunguliwa rasmi

“Haya tunayofanya sasa ni maandalizi, naamini tutafanikiwa na kasi ya zoezi hilo itakuwa na nguvu zaidi pindi muda wake utakapofika,” alisema Sendeu.

Licha wa Ngassa kulipwa vizuri ndani ya klabu ya Azam, mshambuliaiji huyo anayetegemwa pia na timu ya taifa, Taifa Stars ameonekana kutaka kuihama baada ya kumaliza katika nafasi ya tatu na kukosa nafasi ya kushiriki michuano ya kimataifa.

Alikaririwa wiki hii akisema kwamba atakuwa tayari kuihama Azam endapo klabu kama Yanga itafuata taratibu za kumsajili kwani nia yake ni kuona kwamba siku moja anacheza soka la kulipwa nje ya nchi.

Wakati huo huo, Azam iko katika hatua za mwisho za kuwanasa wachezaji wengine wawili kutoka Ghana ambao hucheza nafasi za beki wa kati na mshambuliaji.

Idrissa alisema kuwa watataja majina ya wachezaji hao baada ya kutua nchini mwishoni mwa wiki.

CHANZO: NIPASHE

Posted under:  All Articles

Tags:  

Comments