Stars uso kwa uso na Msumbiji leo

Timu ya soka ya taifa, ‘Taifa Stars’, leo jioni itashuka kwenye Uwanja wa Taifa wa Msumbiji kucheza mechi ya kimataifa ya kirafiki kwa ajili ya ufunguzi wa uwanja huo mpya.

Stars iliyoondoka jana alfajiri na kikosi cha wachezaji 19 imefika salama nchini humo tayari kwa ajili ya mchezo huo maalum.

Akizungumza na NIPASHE, kocha wa Stars, Jan Poulsen alisema kuwa wataitumia mechi ya leo kama sehemu ya maandalizi ya mchezo wao wa marudiano wa kuwania tiketi ya kushiriki fainali za mwakani za Mataifa ya Afrika dhidi ya Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Poulsen alisema kuwa mchezo huo ambao hata hivyo haumo katika kalenda ya FIFA utampa nafasi ya kuangalia mapungufu ya kikosi chake na kuyafanyia kazi kabla ya mechi yao ya marudiano ugenini Afrika ya Kati.

“Hii ni nafasi nzuri ya kuangalia mapungufu ya kikosi, mchezo dhidi ya Msumbiji ni kipimo kizuri kwetu,” alisema Poulsen.

Aidha, alisema kuwa wachezaji aliowaita kwenye kikosi hicho kwa ajili ya mchezo huo wengi wao waliichezea Stars kwenye mchezo wa kwanza dhidi ya Jamhuri ya Afrika ya Kati uliochezwa kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam mwezi uliopita ambapo wenyeji walishinda 2-1.

Naye nahodha wa Stars, Shadrack Nsajigwa, alisema kuwa pamoja na kuwa mchezo huo ni wa kirafiki, wachezaji wamepanga kucheza kiushindani kwa kuwa wana malengo makubwa Afrika.

“Sisi tumejiandaa kwenda kupambana, tunajua ni mchezo wa kirafiki lakini ni muhimu kwetu, sisi tunawaza kufuzu CAN 2012,” alisema Nsajigwa.

Kikosi cha Stars kinategemewa kurejea nchini Jumatatu kujiandaa na mchezo wa marudiano dhidi ya Jamhuri ya Afrika Kati unaotegemewa kucheza Juni mwaka huu nchini humo.

Posted under:  All Articles

Tags:  

Comments