Ulimwengu kuripoti TP Mazembe Ijumaa

TP Mazembe
Image via Wikipedia

Mshambuliaji tegemeo wa timu ya soka ya Tanzania ya vijana wa umri chini ya miaka 23, Thomas Ulimwengu ataondoka nchini keshokutwa kuelekea Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kwa ajili ya kwenda kufanya majaribio ya kucheza soka la kulipwa katika timu ya TP Mazembe. Akizungumza jana, Afisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniface Wambura alisema kuwa Ulimwengu atakuwa huko mpaka Aprili Mosi lakini shirikisho hilo linatarajia kuwapelekea maombi mabingwa hao watetezi wa Afrika kwamba watamhitaji nyota huyo wakati timu ya vijana itakapokwenda Yaounde, Cameroon kuwavaa wenyeji wao Machi 27. Wambura alisema TP Mazembe wamevutiwa na nyota huyo baada ya kumuona katika mechi mbalimbali alizocheza na hiyo inatokana na kuwafuatiliwa kwa muda mrefu wachezaji wa Tanzania kabla hata ya kupangwa kukutana na mabingwa wa Tanzania Bara, Simba ya Dar es Salaam. “Tunaamini TP Mazembe watamruhusu ili aweze kuungana na wenzake kwenda Cameroon na baadaye kurejea Kongo ili kuendelea na majaribio yake, ” alisema Wambura. Ulimwengu ambaye alianza kung’ara akiwa na timu ya mkoa wa Dodoma ya Copa Coca Cola ni mmoja wa nyota wanaolelewa katika kituo cha Tanzania Soccer Academy kinachomilikiwa na TFF. Mshambuliaji huyo aliyekuwa anawaniwa pia na miamba ya soka nchini, Simba na Yanga, alirejea Tanzania kujiunga na kambi ya vijana iliyoko chini ya Jamhuri Kihwelu ‘Julio’ akitokea Sweden ambako anapata mafunzo katika kituo cha soka cha ABC. Endapo Ulimwengu atafuzu majaribio hayo ataweza kuungana na nyota wengine kutoka Zambia na Malawi wanaoichezea timu hiyo yenye mafanikio makubwa hapa barani Afrika. CHANZO: NIPASHE

Posted under:  All Articles

Tags:  

Comments