Kuziona Simba, Yanga 3,000

SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) limetangaza viingilio katika mechi ya marudiano ya Ligi Kuu Bara baina ya mahasimu wa jadi nchini Simba na Yanga unaotarajia kupigwa keshokutwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wambura, alisema kwamba katika mechi hiyo kiingilio cha chini kitakuwa sh 3,000 ambacho kitahusu watakaokaa viti vya kijani mzunguko, ambavyo vina uwezo wa kuchukua watazamaji 19,648 na cha juu VIP A ni sh 30,000 ambavyo vina uwezo wa kuchukua watazamaji 748.

Wambura alitaja viingilio vingine kwa kuwa ni sh.5,000 kwa viti vya bluu mzunguko ambavyo vina uwezo wa kuchukua watazamaji 17,045, huku watakaokaa viti rangi ya chungwa vinavyoingiza watazamaji 11,897 watalipa sh 7,000, wakati VIP C yenye viti 4,060 watalipa sh 10,000 na VIP B lenye viti 4,160 watalipa sh 20,000.

Wambura aliongeza kuwa tiketi hizo zinatarajiwa kuanza kuuzwa kesho kuanzia saa mbili asubuhi katika vituo vya mbalimbali ikiwemo Shule ya sekondari Benjamin Mkapa, Big Bon Msimbazi na mgahawa wa Steers uliopo Mtaa wa Samora/Ohio na Uwanja wa Uhuru.

“Pia siku ya mchezo zitaendelea kuuzwa katika maeneo hayo kuanzia saa mbili asubuhi hadi saa sita mchana na baada ya muda huo zitaendelea kuuzwa katika Uwanja wa Uhuru pekee”, alisema Wambura.

Wambura alisema Oden Mbaga kutoka Dar es Salaam ndiye atakuwa mwamuzi wa mechi hiyo akisaidiwa na Mohamed Mkono wa Tanga na Maxmillian Nkongolo wa Rukwa, huku mwamuzi wa mezani atakuwa Hashim Abdallah, wakati kamishna atakuwa mchungaji, Army Sentimea wa Dar es Salaam.

Posted under:  All Articles

Tags:  

Comments