Simba hatua moja kuivaa Mazembe

Simba jana ilianza vizuri Ligi ya Klabu Bingwa Afrika mwaka huu baada ya kulazimisha sare ya kutofungana na wenyeji Elan de Mitsoudje katika uwanja wa Sheikh Said Mohammed hapa Comoro.

Kwa suluhu hiyo Simba imejiweka katika nafasi nzuri ya kukutana na TP Mazembe ya DR Congo katika mzunguko unaofuata kutokana na kuhitaji hata ushindi wa 1-0 katika mchezo wa marudiano, nyumbani, wiki mbili zijazo.

Kocha wa Simba Patrick Phiri aliridhika zaidi na suluhu hiyo kutokana na wenyeji wanaovaa uzi wa njano kama Yanga kutengeneza nafasi nyingi zaidi za kufunga hasa katika kipindi cha kwanza.

Mussa Hassan Mgosi alikosa bao la wazi mwanzoni mwa kipindi cha pili baada ya kuchelewa kuiwahi krosi ya Rashid Gumbo ambayo ilikatiza mbele ya lango la wenyeji huku mlinda mlango wake akiwa ametoka golini.

Simba ilipoteza nafasi nzuri zaidi ya kufunga baadaye baada ya mpira wa kichwa na Mgosi kugonga mwamba katika dakika ya 65.

Simba ilifanya mabadiliko katika kipindi cha pili ikiwapumzisha Hillary Echesa na nafasi yake kuchukuliwa na Amri Kiemba na pia ikimrudisha benchini Rashid Gumbo na kumuingiza Nico Nyagawa.

Lakini pamoja na mabadiliko hayo, kosakosa ziliendelea langoni mwa wenyeji kipa wa wenyeji akipangua shuti la Jerry Santo dakika 10 kabla ya mpira kumalizika.

Simba: Mustafa Barthez, Haruna Shamte, Juma Jabu, Meshack Abel, Juma Nyosso, Jerry Santo, Hilary Echesa (Amri Kiemba), Rashid Gumbo (Nico Nyagawa), Patrick Ochan, Emmanuel Okwi, Mussa Mgosi.

CHANZO: NIPASHE JUMAPILI
Enhanced by Zemanta

Posted under:  All Articles

Tags:  

Comments