Wachezaji Simba wajazwa mamilioni

Timu ya Simba

Uongozi wa klabu ya Simba umewapa wachezaji wa timu hiyo fedha taslimu Sh. Milioni 10 kama motisha kutokana na ushindi wa 2-0 katika mechi wao wa fainali ya Kombe la Mapinduzi dhidi ya watani wao, Yanga iliyochezwa juzi kwenye uwanja wa Amaan visiwani hapa.

Kutokana na zawadi hiyo, wachezaji wa timu hiyo sasa watagawana jumla ya Sh. Milioni 15 ambazo ni pamoja na zawadi ya Sh. Milioni 5 walizopata kwa kutwaa ubingwa wa michuano hiyo ya kila mwaka.

Akizungumza na NIPASHE jana, Makamu Mwenyekiti wa Simba, Godfrey Nyange ‘Kaburu’ alisema kuwa wamefurahishwa na ushindi huo na wataendelea kuwapa motisha wachezaji katika kila mechi wanazocheza ili kuwaongezea ari.

Kaburu alisema kuwa wanawataka wachezaji wao wajitume katika mazoezi ili waweze kutetea vyema ubingwa wao na kufanya vizuri katika mashindano ya Klabu Bingwa Afrika.

“Tumefurahi sana, tumewapa Sh. Milioni 10 na zile za zawadi zilizotolewa sasa watagawana Sh. Milioni 15,” alisema Kaburu.

Katika hatua nyingine, aliyekuwa Waziri Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Ali Juma Shamhuna, ametangaza kuwapatia wachezaji wa Simba zawadi kutokana na ushindi walioupata.

Shamhuna anatarajiwa kuwaalika wachezaji wa Simba nyumbani kwake kabla ya kurejea jijini Dar es Salaam na anawatakia wakafanye vizuri katika mashindano ya kimataifa.

Mechi hiyo ya watani wa jadi ilivunja rekodi ya mapato katika uwanja wa Amaan baada ya kuingiza Sh. Milioni 27.8. Mapato hayo ni zaidi ya jumla ya mapato ya mechi mbili za nusu fainali zilizozikutanisha timu hizo kubwa nchini dhidi ya Zanzibar Ocean View na Mtibwa ya Morogoro. Mechi ya nusu fainali baina ya Simba dhidi ya Zanzibar Ocean View iliingiza Sh. Milioni 11, wakati iliyoikutanisha Yanga dhidi ya waliokuwa mabingwa watetezi, Mtibwa iliingiza Sh. Milioni 10.

Wakati huo huo, mfungaji wa Simba, Mussa Hassan ‘Mgosi’, amesema kuwa kipigo walichoipa Yanga juzi ni salamu za rasharasha na kwamba mvua kamili wataipata katika mechi yao ya marudiano ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara itakayofanyika Machi 5 kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Mgosi ambaye alifunga goli la kwanza katika dakika ya 33 alisema kuwa wamefurahi kushinda mchezo huo na umewasaidia kuwaimarisha kuelekea katika hatua la lala salama ya ligi ya bara.

Alisema kuwa kila mchezaji amepanga kuonyesha uwezo wa juu katika mechi za ligi na vile vile kuhakikisha wanashinda pia mechi zao za michuano ya kimataifa.

“Tunashukuru Mungu tumeshinda, ni dalili njema kuwa na ligi itakuwa furaha upande wetu,” alisema Mgosi ambaye aliachwa katika kikosi cha timu ya Taifa, Taifa Stars, kutokana na kuwa majeruhi.

Aliongeza kuwa mafanikio na ushindi wa timu yao katika mechi mbalimbali walizocheza yametokana na jitihada wanazozionyesha mazoezini na wanaamini kwamba hali ikiendelea hivyo, hakuna timu itakayoweza kuwavua ubingwa wa ligi ya bara.

“Kila mchezaji Simba anauwezo wa kufanya vizuri, tunajivunia hali hii na wala hatuoni kama tumepungukiwa, tutaendelea kujiimarisha ili tuweze kuiwakilisha nchi vizuri katika mashindano ya kimataifa mwaka huu,” aliongeza Mgosi aliyejiunga na Simba mwaka 2005 akitokea Mtibwa Sugar ya Manungu mkoani Morogoro.

Mwaka huu Simba itaiwakilisha nchi katika mashindano ya Klabu Bingwa Afrika kwa kuanza na klabu ya Elan de Mitsoudje ya Comoro na vile vile mwezi Mei itaiwakilisha Bara katika mashindano ya Kombe la Kagame yatakayofanyika visiwani hapa mwezi Mei.

Katika mchezo wa jana, Simba iliwakosa nyota wake watano ambao walikuwa katika timu ya taifa ambao ni pamoja na Juma Kaseja, Rashid Gumbo, Kevin Yondani, Juma Nyoso, Ali Shiboli huku Okwi Emmanule akiwa mgonjwa na Joseph Owino akiwa kwao Uganda akimalizia mitihani yake.

Yanga nao iliwakosa nyota wake sita walioko Stars ambao ni Nadir HaroubCannavaro‘, Jerry Tegete, Shadrack Nsajigwa, Stephano Mwasika, Nurdin Bakari na aliyekuwa nahodha wao, Abdi Kassim ‘Babi’ ambaye tayari ameuzwa katika klabu mpya ya Dom Tang Long ya Vietnam.

CHANZO: NIPASHE
Enhanced by Zemanta

Posted under:  All Articles

Tags:  

Comments