Poulsen: Kipigo Stars kimetukomaza

Kocha Jan Poulsen amesema kipigo cha 5-1 ilichokipata timu ya taifa ya soka ya Tanzania, Taifa Stars, juzi kutoka kwa mabingwa mara saba wa Afrika, Misri katika mechi yao ya ufunguzi wa michuano ya Kombe la Bonde la Mto Nile kimewakomaza na kitawasaidia kujiamini katika mechi zijazo.

Poulsen alisema kipigo hicho cha pili mfululizo kinachofanana kutoka kwa Mafarao kimewapa somo na kimewaongezea ujasiri wa kukabili timu zijazo kwa sababu “Misri ni timu bora kabisa Afrika”.

“Tumecheza na timu bora, huwezi ukalinganisha nafasi ya 116 tuliyopo Tanzania na wao ambao ni wa tisa kwa bora wa soka duniani, wao pia ndiyo namba moja barani Afrika,” alisema Poulsen baada ya mechi hiyo kwenye Uwanja wa Arab Contractors mjini hapa.

“Misri ni timu nzuri, imecheza vizuri, ni mabingwa mara tatu mfululizo Afrika, vijana wangu walipambana vilivyo, lakini walikutana na timu bora, naamini michezo ijayo tutaimarika,” alisema Poulsen.

Mdenmark huyo alisema kuwa makosa machache waliyoyafanya wachezaji wake yalitumiwa vizuri na wapinzani wao kufunga na hiyo ilitokana na kucheza bila kuelewana katika dakika 20 za kwanza.

“Watanzania tumejifunza mengi kwa mechi ya leo (juzi), faida yake itaonekana katika mechi zijazo,” alisema Poulsen.

Hassan Shehata, kocha wa Misri aliyeisaidia nchi hiyo kutwaa ubingwa wa Afrika mara tatu mfululizo, aliisifu Stars akisema inahitaji marekebisho kidogo.

Shehata alisema soka walilocheza Stars katika kipindi cha pili lilikuwa ni bora na kwamba kama wangecheza hivyo kipindi cha kwanza mchezo ungekuwa mgumu kwao na akaongeza kuwa timu yake licha ya kupata ushindi mnono ilikabiliana na upinzani mkubwa.

Nahodha wa Stars, Shadrack Nsajigwa alisema hali ya hewa ya baridi kali nayo ilichangia kwa kiasi fulani kuwachanganya wachezaji hasa kipindi cha kwanza, lakini baadaye walichangamka wakati mambo yakiwa tayari yameharibika.

Nsajigwa aliwaomba Watanzania wasikatishwe tamaa na matokeo hayo na kukumbusha kuwa hata michuano ya Chalenji iliyomalizika mwezi uliopita jijini Dar es Salaam timu ya Taifa ya Tanzania Bara ‘Kilimanjaro Stars’ ilianza kwa kufungwa bao 1-0 na Zambia lakini ikaja kuwa bingwa.

Naye nahodha wa Misri, Wael Gomaa alisema michuano hiyo ya soka kwa nchi za Bonde la Mto Nile ni migumu na kwamba Tanzania si timu ya kubezwa kwani ina wachezaji wenye miili midogo lakini wana vipaji.

Mvua ya magoli kwa Stars ilianza katika dakika ya nne kupitia kwa Said Khamdi, kiungo Mohammed Aboutrika alifunga la pili katika dakika ya 14 kabla ya beki Nadir HaroubCannavaro’ kujifunga dakika sita baadaye wakati akijaribu kuokoa mpira wa krosi.

Bao la nne lilifungwa na Said Khamdi katika dakika ya 57 na Ahmed Ally alipigilia msumari wa mwisho kwenye ‘jeneza’ la Stars katika dakika ya 74. Stars ilijipangusa machozi kwa goli la dakika ya 77 lililofungwa na mchezaji aliyeenda Misri kibahati Rashid Gumbo wa Simba. Gumbo aliongezwa katika dakika za mwisho kabla ya safari ya kwenda Cairo kuziba nafasi ya Henry Joseph aliyejitoa kikosini kutokana na matatizo binafsi.

Stars itatupa karata yake ya pili kesho dhidi ya Burundi, ambayo nayo juzi ilifungwa mabao 3-1 na Uganda. Stars itamaliza hatua ya makundi kwa kucheza dhidi ya Uganda.

Michuano hiyo inashirikisha nchi saba zilizogawanywa katika makundi mawili, ambapo timu mbili za juu kila kundi zitacheza nusu fainali, wakati timu zitakazoshika nafasi ya tatu katika kila kundi zitacheza kuwania mshindi wa tano. Bingwa wa michuano hiyo atazawadiwa zaidi ya Sh. Milioni 250 za Tanzania.

CHANZO: NIPASHE
Enhanced by Zemanta

Posted under:  All Articles

Tags:  

Comments