Stars yabakiza Kombe Chalenji

Penati ya Tony Maweja iliyodakwa kiustadi na kipa Juma Kaseja iliisaidia timu ya taifa ya Tanzania Bara’Kilimanjaro Stars’ kutinga fainali ya Kombe la Chalenji baada ya kushinda kwa penati 5-4 katika mechi yao ya nusu fainali dhidi ya Uganda kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam jana.

Stars waliokuwa wakicheza kwa kujituma zaidi jana na kutengeneza nafasi kadhaa za kufunga katika kipindi cha pili, walisimama imara dhidi ya mabingwa watetezi Uganda na hatimaye kumaliza dakika 90 za kwanza kwa sare ya 0-0.

Kabla ya kumalizika kwa dakika za kawaida, Stars timu zote zilifanya mashambulizi kadhaa ya hatari, zikiwemo walizokosa Stars kupitia kwa Mrisho Ngassa katika dakika ya tatu na dakika ya 70 huku Uganda wakikumbukia nafasi ya wazi ya dakika ya 49 wakati mpira wa kichwa wa Mike Serumanga ulipopanguliwa na Kaseja.

Dakika 30 za nyongeza hazikutoa mshindi na ndipo ikafikia hatua ya kupigiana penati ‘tano-tano’, ambapo Stars iling’ara baada ya wachezaji wake kufunga penati zote kwa ufundi, huku kipa Kaseja akiwapa raha zaidi Watanzania na kurahisisha ushindi baada ya kuokoa penati ya nne.

Kipa Odongkara Robert wa Uganda alishindwa kudaka penati zilizojaa wavuni za nahodha Shadrack Nsajigwa, Stephano Mwasika, Shaaban Nditi, Salum Machaku na Erasto Nyoni.

Penati nne za Uganda zilifungwa na Isinde Isaac, Walusimbi Godfrey, Emmanuel Okwi na Andrew Mwesigwa.

Kutokana na ushindi huo, Stars wamefanikiwa kulibakisha kombe la Chalenji nchini, kwani wanafainali wenzao, timu ya Ivory Coast ambayo ilishinda 1-0 katika nusu fainali ya kwanza dhidi ya Ethiopia jana, si wanachama wa shirikisho la soka la Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) na wanashiriki wakiwa ni waalikwa, kama walivyokuwa wenzao wa timu ya taifa ya Zambia.

Hata hivyo, kama Ivory Coast watashinda dhidi ya Stars, watakabidhiwa zawadi ya mshindi wa kwanza ya kitita cha dola za Marekani 30,000 na Stars watakabidhiwa kombe la ubingwa wa mwaka huu.

FAINALI KIINGILIO SH 1,000

Viingilio vya mechi ya fainali ya Kombe la Chalenji itakayochezwa kesho kwenye Uwanja wa Taifa kati ya Stars na Ivory Coast kitaendelea kuwa kilekile cha Sh. 1,000 hadi Sh. 5,000 kwa viti vya VIP ‘A’.

Kaimu Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Sunday Kayuni, aliwaambia waandishi wa habari mara baada ya mechi ya Stars na Uganda jana kuwa wameamua kuacha viingilio hivyo ili Watanzania wengi zaidi wapate nafasi ya kwenda kuishangilia timu yao.

Kayuni alisema vilevile kuwa kesho, mechi ya kwanza ya kumsaka mshindi wa tatu kati ya Uganda na Ethiopia itaanza saa 7:30 mchana na tiketi za mechi ya fainali zitaanza kuuzwa leo saa 5:00 asubuhi.

Katika hatua nyingine, kikosi cha Stars kimepata pigo baada ya mshambuliaji Mrisho Ngassa kupata kadi ya pili ya njano jana.

CHANZO: NIPASHE
Enhanced by Zemanta

Posted under:  All Articles

Tags:  

Comments