Maelfu wamzika kocha Mziray

Mwenyekiti wa Chama cha Muziki wa Dansi Tanzania, Kassim Mapili akiweka shada la maua kwenye kaburi la aliyekuwa kocha wa soka, Syllersaid Mziray ambaye alizikwa katika makubiri ya Kinondoni jijini Dar es Salaam jana. (Picha: Tryphone Mweji) Maelfu ya mashabiki wa soka walijitokeza jana kwenye makaburi ya Kinodnoni jijini Dar es Salaam kumzika aliyekuwa kocha wa klabu ya Simba, marehemu Syllersaid Salmin Kahema Mziray. Mwili wa kocha huyo aliyewahi pia kuzifundisha timu za African Sport ya Tanga, Pilsner, Yanga na timu ya taifa, Taifa Stars, ulizikwa jana na kuhudhuriwa pia na vigogo kadhaa, wakiwemo Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Joel Bendera, Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) Leodgar Tenga na viongozi wa juu wa klabu yake ya Simba na pia watani zao wa jadi, Yanga. Mashabiki wa soka walishiriki kuuaga mwili wa marehemu kuanzia saa 6:30 mchana na kumzika saa 10:00 jioni. Awali, Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, George Mkuchika, alituma salamu za rambirambi na kusema kuwa yeye na Serikali wamesikitishwa na msiba huo na kuwapa salamu za pole wanafamilia wa marehemu. Tenga alimuelezea Mziray kwamba, alikuwa kocha makini, mtetezi wa hoja alizoamini kuwa ni sahihi na ambaye alikuwa na utaalam uliokuwa muhimu kwa taifa. Makamu Mwenyekiti wa Simba, Godfrey Nyange ‘Kaburu’, alisema Mziray alikuwa ni mchapa kazi hodari na, alikiri kwamba wataukosa sana mchango wake. Mwenyekiti wa Yanga, Lyody Nchunga, aliwapa pole wenzao wa Simba na kusema kwamba utaalam wa Mziray ulikuwa na umuhimu mkubwa kwa maendeleo ya soka nchini. Mazishi hayo pia yalihudhuriwa na Mwenyekiti wa Baraza la Michezo Tanania (BMT), Idd Kipingu na Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo (TASWA), Juma Pinto. Kabla ya kifo chake, Mziray alikuwa kiifundisha Simba na pia alikuwa mhadhiri wa Chuo Kikuu Huria Tanzania (OUT). Mungu ailaze roho ya Mziray mahala pema peponi. Amin! CHANZO: NIPASHE

Enhanced by Zemanta

Posted under:  All Articles

Tags:  

Comments