Twiga Stars wajazwa mamilioni

Timu ya taifa ya soka ya wanawake Tanzania, Twiga Stars

Timu ya taifa ya soka ya wanawake Tanzania, Twiga Stars, jana ilipokea msaada wa fedha zaidi ya Sh. Milioni 92 kwa ajili ya kufanikisha safari ya kuelekea Gaborone, Botswana na baadaye Afrika Kusini kushiriki fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa wanawake zitakazoanza Oktoba 31.

Msaada huo unatoka kwa Kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL) waliotoa Sh. Milioni 83.1, wakati waliokuwa wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Spika wao, Samuel Sitta, waliichangia Sh. Milioni 8.9.

Akizungumza jana, Meneja Bidhaa wa SBL, Nandy Mwiyombewa alisema kampuni yake imeamua kutoa msaada huo kwa kuthamini maendeleo ya timu hiyo.

Mwiyombewa alisema pia SBL imetoa vifaa vyenye thamani ya Sh. Milioni 14 kwa ajili ya kuvitumia kwenye michuano hiyo na inawatakia mafanikio katika ushiriki wao.

Naibu Waziri wa Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo, Joel Bendera, aliyekuwa akikabidhi bendera kwa timu hiyo, alisema kuwa kutokana na jitihada zilizoonyeshwa na wachezaji wa Twiga Stars, waliamua kuwaomba msaada wabunge na hicho kilichopatikana kimetokana na wachache waliokubali kuwachangia.

Hata hivyo, Bendera hakuwa tayari kutaja majina ya wabunge waliochangia licha ya kwamba wameweka saini zao katika karatasi la mchango, na akawataka wachezaji wa timu hiyo kuhakikisha wanaiwakilisha vyema nchi.

Alisema kuwa kazi kubwa ilikuwa ni kupata tiketi ya kushiriki fainali hizo na sasa kilichobaka ni kuhakikisha wanashinda na kuipa heshima nchi.

“Tumechoka kushindwa, tunataka ushindi, tusiende kichwa chini, na tusiwe na visingizio, kila kitu mmekamilishiwa,” Bendera aliwaeleza wachezaji wa timu hiyo.

Aliwataka watumie vyema ufundi, ujanja na mbinu zote za ushindi walizopewa na makocha wao na kwamba wakitekeleza hayo watarejea nyumbani na ubingwa wa mashindano hayo na kuweka rekodi mpya ambayo haijawahi kuwekwa nchini.

Kocha Mkuu wa timu hiyo, Boniface Mkwasa alisema kuwa wachezaji wake wameiva na baada ya motisha waliyopokea anaamini watakuwa makini ili kutekeleza kile walichoelezwa.

Mkwasa alisema kuwa ingawa mashindano ni magumu, vijana wake wameimarika na muda mrefu waliokuwa kambini alikuwa akiwapa mazoezi mara tatu kwa siku ili kuwajengea ukakamavu na uvumilivu.

Naye nahodha wa timu hiyo, Sophia Mwasikili, alisema kuwa wanaenda Afrika Kusini kushindana na wanawaomba Watanzania wawaombee dua ili watimize malengo yao.

“Tunaenda kushindana, tuna imani tutafanya vizuri, tunawashukuru wote waliokuwa pamoja na sisi kuanzia mwanzo,” aliongeza beki huyo wa kushoto.

Katika mashindano hayo, Twiga Stars iko ‘Kundi la Kifo’ pamoja na wenyeji Afrika Kusini, Mali na mabingwa mara tano wa michuano hiyo iliyofanyika mara sita, Nigeria.

CHANZO: NIPASHE
Enhanced by Zemanta

Posted under:  All Articles

Tags:  

Comments