Sina mkataba Yanga – Papic

Kocha wa Yanga, Mserbia, Kostadin Papic

Kocha wa Yanga, Mserbia, Kostadin Papic, amefichua kuwa mkataba wake na ‘Wanajangwani’ aliosaini mwaka jana umemalizika na hivi sasa anafanya kazi kama kibarua.

Papic ambaye alijiunga na Yanga baada ya Mserbia mwenzake Dusan Kondic kuachia ngazi, alimaliza mkataba wake mapema mwezi huu.

Akizungumza na NIPASHE jana, Papic alisema kuwa kabla ya mkataba huo wa mwaka mmoja kumalizika, alianza mazungumzo na uongozi lakini hadi sasa hawajafikia tamati ya mazungumzo hayo.

Zaidi ya hayo, Papic aliiambia NIPSHE kuwa licha ya kutoafikiana na uongozi hadi sasa juu ya mkataba mpya, pia kuna mambo ya kiufundi ambayo amewaeleza wayatekeleze kwa ajili ya maendeleo ya timu yao lakini bado hayajafanyiwa kazi.

“Tangu Agosti tumekuwa na mazungumzo lakini hayatekelezwi… kwa sasa, niko huru, sina mkataba na Yanga,” alisema kocha huyo.

Aliongeza kuwa hali hiyo imemfanya kutokuwa na programu za muda mrefu kwa timu yake na kutekeleza kila kinachohitajika kwa wakati husika, jambo ambalo anaamini si zuri kwa maendeleo ya timu.

“Kuna wakati huwa nakumbana na hali ngumu, utendaji wao ndio tatizo kwa sababu utekelezaji huwa unachelewa,” aliongeza kocha huyo ambaye Jumamosi iliyopita aliisaidia Yanga kushinda 1-0 dhidi ya watani zao Simba, ikiwa ni ushindi wa pili mfululizo baada ya kuwahi kuwaliza pia kwa penati 3-1 katika mechi yao ya Agosti ya kuwania Ngao ya Jamii.

Papic aliongeza kuwa baada ya kurejea jijini Dar es Salaam akitokea Mwanza, alikuwa na mazungumzo tena na uongozi wa klabu hiyo kuhusiana na hatma yake na maandalizi ya mechi ijayo dhidi ya JKT Ruvu itakayochezwa keshokutwa kwenye uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro.

“Kama hatutafikia makubaliano, naweza kuiacha Yanga… na kesho nina mpango wa kuzungumza na vyombo vya habari,” aliongeza kocha huyo aliyetua barani Afrika mwaka 2000 kufundisha klabu kubwa kadhaa zikiwemo za Kaizer Chiefs na Orando Pirates za Afrika Kusini, Enyimba na Enugu za Nigeria na Asante Kotoko na Hearts of Oak za Ghana.

Akizungumza na NIPASHE kuhusiana na mkataba wa Papic, Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Davis Mosha, alisema kuwa tayari uongozi wa klabu hiyo umeshafanya mazungumzo na kilichobaki sasa ni utekelezaji wa makubaliano yao.

Katika mkataba uliomalizika, Papic ambaye aliwahi kutuma maombi ya kuifundisha timu ya taifa, Taifa Stars baada ya mkataba wa Mbrazil Marcio Maximo kumalizika, analipwa mshahara wa mwezi wa Dola za Marekani 10,000 (sawa na Sh. Milioni 14.9) na posho mbalimbali za kujikimu.

Wakati huo huo, kocha wa Simba, Patrick Phiri, ameondoka nchini na kurejea kwao Zambia kutokana na kile kilichoelezwa kuwa ni kwenda kumuuguza mkewe.

Akizungumza na gazeti hili jana, Makamu Mwenyekiti wa Simba, Godfrey Nyange ‘Kaburu’, alisema uongozi wa klabu yao umempa Phiri ruhusa ya kwenda kumuuguza mkewe na kwamba atarejea nchini baada ya hali ya mgonjwa wake kutengemaa.

Hivi karibuni, Phiri pia aliondoka pia na kwenda kwao baada ya kupata taarifa za msiba wa binamu yake.

Kila kocha Phiri anapolazimika kwenda kwao, mashabiki wa Simba huingiwa na hofu kuwa huenda asirudi tena, kwani alishawahi kuiacha Simba kwa staili kama hiyo.

Alipotafutwa jana, kocha huyo hakupatikana baada ya simu yake ya mkononi kujibu mara kadhaa kuwa imezimwa.

CHANZO: NIPASHE
Enhanced by Zemanta

Posted under:  All Articles

Tags:  

Comments