Taifa stars kutajwa leo..kila la kheri

Wakati kocha wa timu ya taifa ya soka, Taifa Stars, Jan Poulsean, akitarajiwa kutangaza leo majina ya wachezaji 18 watakaoikabili Morocco katika mechi ya kuwania kufuzu kwa fainali za Mataifa ya Afrika 2012, shirikisho la soka nchini (TFF) limesema viingilio katika mechi hiyo vitakuwa bei poa.
Kocha Poulsen, ambaye awali alitangaza kikosi cha wachezaji 23, alipungukiwa nyota mmoja siku moja tu baada ya kuingia kambini kufuatia kushindwa kufanya mazoezi kwa mshambuliaji wa Simba, Mussa Hassan ‘Mgosi’ kutokana na kuwa majeruhi, aliahidi kubaki na wachezaji 18 kwa ajili ya mechi hiyo.
Poulsen alitarajiwa kupitisha ‘panga’ la kikosi chake jana, lakini alitumia muda wake kushiriki kwenye uzinduzi wa kampeni ya ‘Shangilia Stars’ inayoendeshwa na kampuni ya bia ya Serengeti, ambao ni miongoni mwa wadhamini wa timu hiyo ya taifa.
Akizungumza kwenye uzinduzi huo, Rais wa TFF, Tenga alisema kuwa shirikisho hilo la soka litapanga viingilio vya chini ili kila Mtanzania mpenda soka aweze kuhudhuria na kuisapoti timu hiyo.
Alisema kuwa mashabiki wana mchango wao mkubwa katika kuisaidia timu hiyo ishinde mechi hiyo dhidi ya wao Morocco, ambao wanatarajiwa kutua jijini Dar es Salaam Ijumaa na kufikia katika hoteli ya Kilimanjaro Kempinski kwa ajili mechi hiyo ya Jumamosi.
Tenga alisema Stars wanao uwezo wakupata matokeo mazuri kwenye mechi hiyo itakayochezwa kwenye Uwanja wa Taifa.
“Tuliweza kutoka sare ugenini dhidi ya Algeria, hatuwezi kushindwa hapa nyumbani, vijana wetu wanao uwezo na ari ya kushinda,” alisema Tenga.
Uzinduzi wa kampeni ya ‘Shangilia Stars’ ulihudhuriwa pia na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais Anayeshughulikia Muungano, Muhammed Seif Khatib, pamoja na wachezaji wa timu ya Taifa.
Wakati huo huo, beki wa kati wa Stars, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ aliiambia NIPASHE jana kuwa
kuwa wachezaji wameandaliwa vizuri kwa ajili ya mechi hiyo na kwamba wamedhamiria kuwashangaza Wamorocco.
“Hatutawaangusha Watanzania, tunachoomba ni sapoti yao ili tuweze kushinda, hatuwahofii wapinzani wetu, tutaenda nao sahani moja,” alisema beki huyo wa klabu ya Yanga.
Mshambuliaji wa Stars, Danny Mrwanda, ambaye hakuwa na mengi ya kusema, aliwataka Watanzania wajitokeze kwa wingi kwenye mechi hiyo akisema jambo hilo litawaongezea wachezaji hali ya kujiamini.
Wachezaji walioitwa ni:
Makipa: Juma Kaseja (Simba), Shaban Kado (Mtibwa) na Said Mohammed (Majimaji)
Mabeki: Aggrey Moris, Erasto Nyoni (Azam FC), Nadir Haroub, Shadrack Nsajigwa, Stephano Mwasika (wote kutokaYanga), Haruna Shamte (Simba), na Salmin Kiss kutoka Polisi Dodoma.
Viungo: Henry Joseph (Kongsvinger ya Norway), Shaban Nditi, Salum Machaku (wote kutoka Mtibwa), Nurdin Bakari (Yanga), Jabir Aziz, Seleman Kassim (wote kutoka Azam FC), Nizar Khalfan (Vancouver, Canada) na Idrisa Rajabu (Sofapaka, Kenya).
Washambuliaji: Danny Mrwanda (DT Long An, Vietnam), Mohammed Banka (Simba), Mrisho Ngasa na John Bocco (wote Azam FC).

Posted under:  All Articles

Tags:  

Comments