Yanga yaivimbia Serikali

Timu ya Yanga.

Licha ya serikali kuitaka Yanga itafute uwanja mwingine kwa ajili ya mechi zake za Ligi Kuu ya Tanzania Bara juzi, uongozi wa klabu hiyo umesema jana kuwa haujakata tamaa na umepeleka maombi mapya Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo ili waruhusiwe kutumia Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Akizungumza jana mchana, Mwenyekiti wa klabu hiyo, Lloyd Nchunga, alisema kuwa Yanga imefikia maamuzi hayo baada ya kurejea mazungumzo ya awali na serikali ambao ndio wamiliki wa uwanja na kufikia hatua ya kukubaliwa.

Nchunga alisema kuwa endapo wizara hiyo itashindwa kutoa kibali cha kutumia uwanja huo kwa klabu yake hadi kufikia leo saa 10:00 jioni, wataamua kuhamishia mechi zao kwenye uwanja wa Jamhuri mkoani Morogoro.

Aliongeza kuwa Yanga imesikitishwa na maamuzi ya awali ya kuwanyima kutumia uwanja huo, ilhali klabu yao ndiyo ilikuwa timu pekee iliyokubali kutekeleza maelekezo yote yaliyotolewa wakati wakikutana kwa zaidi ya mara tano.

“Wizara inahitaji kuelewa kwamba uwanja huo ni moja ya vitega uchumi ambavyo vinatakiwa kutumika ili kurejesha fedha zilizotumika wakati wa ujenzi na hatimaye kujiendesha wenyewe,” alisema mwenyekiti huyo.

Aliongeza kuwa Yanga pia inashangazwa na maamuzi ya wizara hiyo kubadili msimamo wake wa awali wa kuwaruhusu kutumia uwanja huo baada ya wao kurejea peke yao na kufanya nao mazungumzo.

Alisema kuwa Yanga inashangazwa kuona kwamba imenyimwa ruhusa ya kutumia uwanja huo bila ya kuelezwa sababu za msingi za kutopata kibali cha kuuchezea uwanja huo wenye uwezo wa kuingiza watazamaji 60,000 walioketi.

“Tuliwataka pia TFF watusaidie kutuombea uwanja huo baada ya Simba na Azam kutangaza kutumia viwanja vingine mikoani… na tulikuwa tayari kutekeleza yote wanayoyataka, maamuzi mapya yaliyotolewa na TFF jana (juzi) tumeyapokea kwa masikitiko makubwa,” alisema Nchunga.

Alisema kuwa wao waliendelea na maombi ya kutumia uwanja huo baada ya klabu za Simba na Azam kutotokea katika vikao hivyo, ambapo Yanga ilifikia maamuzi ya kukubali kulipa gharama ambazo wangepaswa kulipa kabla ya makato mengine hayajafanyika na hata kulipia gharama hizo pale ambapo mapato yatakapokuwa madogo.

Alitaja gharama ambazo walielezwa na Wizara kuwa ni Sh. milioni tatu kwa ajili ya Wachina ambao hulipwa katika kila mechi, Sh. Milioni 1.9 (usafi), Sh. 450,000 (alama za uwanjani) na kukatwa asilimia 10 ya fedha zitakazobakia.

Alisema kuwa tayari walielezwa kuwa wangetumia uwanja huo kwa mechi tano kama vile ambavyo wizara hiyo ilikuwa tayari kwa kuzigawanya kwa klabu hizo tatu zilizoomba kutumia uwanja huo.

Hata hivyo, baada ya Yanga kuelekea kupata uwanja huo, watani zao, Simba walitokea katika kikao kingine na kudai kwamba wao pia wanahitaji kuutumia uwanja huo, jambo ambalo lilikataliwa na TFF waliowaeleza kwamba wanaitambua barua yao ya kuhamia Mwanza kwenye uwanja wa CCM, Kirumba.

Jana, Nipashe ilimtafuta Mkurugenzi wa Michezo nchini ambaye ndiye alikuwa mwakilishi wa wizara katika vikao hivyo kwa ajili ya kutoa ufafanuzi, lakini hakupatikana ofisini kwake na vile vile hakupokea simu yake ya mkononi.

Yanga haikuwa na barua yoyote iliyoonyesha kufikia makubaliano na wizara hiyo kama ambavyo TFF ilivyojibiwa na wizara hiyo kwamba haijatoa kibali cha klabu hiyo kutumia uwanja huo.

Leo saa 11:00 jioni ndio mwisho wa Yanga kuwasilisha jina la uwanja ambao itatumia katika mechi zake na Morogoro wanakotaka kuhamia, tayari timu za JKT Ruvu, African Lyon na Ruvu Shooting zimeshauchagua huku Mtibwa Sugar ikiwa ndio mwenyeji pekee wa uwanja huo kwa mechi zinazowahusisha na Simba na Yanga.

CHANZO: NIPASHE
Enhanced by Zemanta

Posted under:  All Articles

Tags:  

Comments