Tukifanya michezo sehemu ya maisha tutafanikiwa  Send to a friend
Monday, 06 September 2010 08:57
0diggsdigg

Allan Goshashy

SIKU hizi michezo ni ajira. Kati ya watu weledi wanaolipwa zaidi duniani hivi sasa ni wanamichezo wa kike na kiume.

Hata waandishi wa habari za michezo na burudani tunapata ujira wetu kwa kuandika taarifa mbalimbali zinazowahusu wanamichezo.

Makocha, madaktari, viongozi wa michezo, wadhamini wa michezo, familia za wanamichezo na nchi pia hunufaika na mafanikio ya wanamichezo na michezo kwa ujumla.

Kwa maana hiyo, nchi haiwezi kutambulika bila ya kuwa na utamaduni wake na mojawapo ya viungo muhimu katika utamaduni wa kila jamii ya binadamu duniani ni michezo.

Michezo ni muhimu katika kuendeleza jamii, pia katika kutambulisha taifa, kutoa burudani, kujenga na kukomaza afya ya mwili na akili na kujenga nidhamu.
Ukiacha michezo ya shule za sekondari (UMISSETA) iliyofanyika nchini mwaka huu, kwa muda wa miaka 10 nyuma michezo hiyo pamoja na ile ya shule za msingi ilikuwa imefutwa kwenye shule, ambapo mpaka sasa michezo ya shule za msingi ( UMITASHUMTA) haijaweza kurudishwa licha ya ahadi za serikali.

Kufutwa kwa michezo hii kwenye shule kwa kiasi kikubwa kumechangia kulikosesha taifa wanamichezo weledi na kusababisha watoto na vijana wengi kuacha shughuli za michezo hata kufanya tu mazoezi kwa ajili ya afya zao.

Ni wazi mtoto anatakiwa akuzwe kielimu na vipaji vyake viendelezwe shuleni kwa sababu waswahili husema, samaki mkunje  angali mbichi.

Ili  kuendeleza vipaji vya watoto na kuwaendeleza kielimu ni lazima sasa tuwe na mtaala wa elimu na mtaala wa ziada (extra curriculum) unaohusu masomo nje ya darasa ambao uwe wa  lazima katika shule na kila mzazi lazima aambiwe wakati akimuandikisha mtoto wake shule ili aweze kuchangia utekelezaji wa mtaala huo.

Mtaala huu wa ziada unatakiwa kuwa wa michezo, muziki na maigizo, na utunzaji wa mazingira, na wanafunzi wafundishwe mtaala huu wa ziada kwa nadharia na vitendo.

Kilele cha hayo yote yawepo mashindano ya michezo, mashindano ya muziki na maigizo na mashindano ya utunzaji wa mazingira,  ambapo mashindano hayo yatafanyika kati ya shule na shule, ngazi ya wilaya, mkoa na kitaifa kila mwaka.

Mtaala huu wa ziada kwa mtazamo wangu ni kwamba ili uweze kufanikiwa serikali inatakiwa itenge bajeti kubwa kwa dhati kupitia wizara yake ya elimu.

Pia, kila shule lazima iwe na viwanja vya michezo, walimu wa michezo, walimu wa mazingira, walimu wa maigizo na muziki, mabasi ya kuwasafirisha wanafunzi, kumbi na eneo la kutunza mazingira.

Mashindano ya mtaala wa ziada yanapofikia katika ngazi ya wilaya, wakuu wa shule wanatakiwa kwenda kwenye ofisi ya wilaya ili kuwatafutia mdhamini wa katika wilaya hiyo kwa sababu ni rahisi kwa serikali kupewa udhamini.

Pia, mkoa unatakiwa utafute udhamini mashindano yanapofikia ngazi ya mkoa na mashindano yanapofikia ngazi ya taifa, wizara inayohusika na elimu pamoja na ile ya michezo, ndizo zitafute mdhamini na kuhakikisha inapanga ratiba tofauti ya mashindano hayo matatu kuanzia ngazi ya chini.

Mtaala huu wa ziada unatakiwa uwe kwenye shule za msingi, sekondari na kwenye vyuo mbalimbali hadi vile vikuu.

Ili mtaala wa ziada uweze kufanikiwa, zipo njia tatu zinazoweza kutumika, kwanza shule lazima iwe na bajeti ya mtaala wa ziada kulingana na uwezo wake na kuamua michezo ya kuipa kipaumbele kutokana na mazingira yake.

Pili wizara ya elimu, wizara ya tawala za mikoa na serikali za mitaa(Tamisemi ), wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo na Idara ya Mazingira (Ofisi ya Makamu wa Rais) lazima zisimamie mtaala huo kwa sababu unahitaji maeneo, utaalamu, ratiba n.k.

Tatu, wadhamini ni muhimu katika kufanikisha mashindano katika ngazi tofauti.

Watanzania kwa upande wetu tunatakiwa tukubali mtaala huu wa ziada tunauhitaji katika kuhakikisha tunaendeleza vipaji vya watoto katika michezo, utunzaji wa mazingira na muziki na maigizo.

Kwa sababu ya kukosekana kwa mtaala huu, wazazi wengi hawapendi pia watoto wao washiriki kwenye michezo kwa sababu wanafahamu mfumo wetu wa michezo kitaifa hautamsaidia mtoto wake maishani.

Lakini, ukweli tatizo lipo katika msingi wa michezo nchini, kwamba hatuna msingi mzuri wa kuandaa wanamichezo weledi, wanamichezo bora wa taifa, wenye uwezo wa kuendeleza taaluma ya michezo nchini.

Pia, watoto wengi hawafahamu umuhimu wa utunzaji wa mazingira na hivyo kusababisha wanapokuwa wakubwa kuharibu mazingira kwa sababu hawajui umuhimu wake au kujua umuhimu wa kutumia mazingira kupata kipato kutokana na kutokuwa na msingi mzuri wa utunzaji wa mazingira.

Vilevile, watoto wanaopenda muziki na maigizo wanaonekana ni wahuni na kazi za muziki hazithaminiwi nchini huku kazi ya maigizo ikionekana kupoteza mwelekeo kwa sababu ya kukosekana msingi imara wa kuandaa waigizaji na wanamuziki.

Ni imani yangu kwamba tutapata wanamichezo weledi na walio bora kama tukiwa na msingi imara wa uandaaji wa wanamichezo, na njia kuu ya kuandaa wanamichezo weledi ni kuanzisha mtaala wa ziada katika shule zetu ambao utakuwa wa michezo, utunzaji wa mazingira na maigizo na muziki.

Pia, kama mtaala wa ziada utaanzishwa, ufuatiliaji wa utekelezaji mtaala huo ni muhimu kama ulivyo ufuatiliaji wa utekelezaji wa mtaala wa elimu, na watoto watakaofanya vizuri kila mwaka kwenye mashindano ya mtaala wa ziada wapewe tuzo.

Posted under:  All Articles

Tags:  

Comments