Twiga Stars yapata mechi za majaribio

TIMU ya soka taifa ya wanawake, Twiga Stars itacheza mechi minne za kirafiki za kimataifa kwa ajili ya kujiandaa na Fainali za Afrika kwa wanawake zitakazofanyika Afrika Kusini baadaye Oktoba.

Twiga Stars itajinoa dhidi ya Afrika Kusini ‘Banyana Banyana’ iliyoilaza mabao 6-0 katika mchezo wa kirafiki mapema mwezi uliopita na baadaye itacheza na Zimbabwe.

Timu  hiyo itacheza na ile ya Afrika Kusini, Septemba 29 nchini na kisha kurudiana Oktoba 2 ugenini kabla ya kucheza na  Zimbabwe, Oktoba 6 na kurudiana  Oktoba 9 mjini Harare.

Mechi hizo ni mahususi kwa timu hiyo  inayojiandaa  na fainali  za soka za wanawake ambazo zitafanyika baadaye mwaka huu nchini Afrika Kusini.

Kocha  wa timu hiyo, Charles Boniface Mkwasa alisema kikosi hicho kinahitaji maandalizi zaidi kwa vile wanashiriki mashindano magumu na yenye manufaa makubwa kwao hivyo kuhitaji maandalizi mazuri .

Alisema wakati timu hiyo ikiwa ziarani Marekani walijifunza mbinu nzuri zikiwamo kasi na ufundi wa kumiliki mpira  ambazo watazitumia vyema mechi hizo za kirafiki kwa ajili ya kuandaa kikosi hicho.

Mkwasa alisema wamepata barua kutoka kwa timu ya Banyana Banyana kuwaomba kushiriki mchezo huo wa kirafiki ambao utachezwa nchini na baadaye kurudiana kwao ambapo gharama zote watalipia na kuwataka wachezaji hao kutumia michezo hiyo kujipanga vyema.

“Tumejifunza mbinu nyingi katika ziara yetu nchini Marekani na ninaamini michezo tutakayocheza itatupa mwanga zaidi wa kujiandaa vyema na fainali zilizo mbele yatu…kikubwa nataka wachezaji wangu wajenge kujiamini zaidi ma wajue wanakwenda kushiriki mashindano makubwa ambayo ndio mara yao ya kwanza,”alisema Mkwasa.

Mkwasa aliwataja wachezaji wa Twiga Stars walioingia kambini jana kuwa ni pamoja na nahodha, Sophia Mwasikili, Fatuma Omary, Mwanaidi Tamba, Fatuma Bushiri, Mwajuma Abdalah, Asha Rashid, Mwanahamisi Omary, Pulkeria Chalagi, Esther Chabruma, Hellen Peter na Fridiana Daudi,

Wengine ni Zena Rashid, Etoo Mlenzi, Mary Masatu, Fatuma Salum, Maimuna Said, Fadhila Hamad, Neema Kuga, Mwasiti Ramadhan, Zuhura Kabulule, Mariam Aziz, Fatuma Mustapha, Evelin Senkubo na  Elizabert Komba.

Enhanced by Zemanta

Posted under:  All Articles

Tags:  

Comments