Yanga bingwa wa Jamii

Tumeua mnyama…Wachezaji wa Yanga wakishangilia baaada ay kukabidhiwa Ngao ya Hisani 2010 baada ya kuwafunga Simba kwa penalti 3-1 kweney uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam jana.(Picha: Khalifan Said).

Yanga jana ilifufua matumaini ya msimu mpya wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara baada ya kuwafunga mahasimu wao wakubwa, Simba, mabao 3-1 katika mechi ya Ngao ya Jamii iliyoamuliwa kwa ‘matuta’ baada ya dakika 90 za mchezo kumalizika kwa sare ya 0-0.

Kwenye Uwanja wa Taifa, ambao haukujaa kama ilivyotarajiwa, Yanga walipata penalti zao za ushindi kupitia kwa Gofrey Bonny, Stephano Mwasika na Isack Boakye, wakati Simba walipata penalti moja tu iliyofungwa na kiungo wa zamani ya Yanga, Mohammed Banka.

Mghana, Ernest Boakye alikuwa mpigaji pekee wa Yanga aliyeshindwa kufunga baada ya penalti yake kupanguliwa na kipa wa Simba, Ali Mustapha ‘Barthez’, wakati wachezaji wa Simba waliopoteza penalti zao walikuwa, Emannuel Okwi, ambaye penalti yake ilipanguliwa, Uhuru Selemani aliyepiga juu na Amri Kiemba aliyegongesha mwamba.

Zilizuka shamrashamra za wana Yanga uwanjani na nje ya uwanja baada ya ushindi huo, dhidi ya timu ambayo imekuwa ikiwanyanyasa sana katika miaka mingi ya karibuni.

Bendera za rangi ya njano na kijani zilipepepea kila kona ya mji, huku magari yakipiga honi mfululizo za kushangilia barabarani, wakati misusuru mirefu ya mashabiki wa Yanga ikitoka uwanjani kwa furaha, huku wana Msimbazi wakiona safari ya kurejea makwao ni ndefu kuliko ilivyo kawaida.

Simba walioonekana kupania zaidi maandalizi ya msimu huu mpya kwa kuajiri makocha wanne, Mzambia Patrick Phiri, Syllersaid Mziray, Seleman Matola na Amri Said ‘Jaap Stam’, ndio waliokuwa wa kwanza kugonga hodi langoni mwa Yanga katika dakika ya 3, wakati ya Nicco Nyagawa iliyomlenga Mussa Hassan ‘Mgosi’ ilipoonekana kuwa tishio, lakini mfungaji bora huyo wa msimu uliopita alishindwa kuuwahi na kumpa nafasi kipa wa Yanga Yaw Berko ‘kuokota’ mpira.

Yanga walijibu mashambulizi hayo dakika mbili baadaye wakati kiungo wao Nsa Job alipomzungusha beki wa Simba Joseph Owino na kumtoka lakini shuti alilopiga lilitoka nje kwa kukosa mmaliziaji.

Simba walibisha hodi tena langoni mwa Yanga katika dakika ya 22 kufuatia ‘gonga’ baina ya Mohammed Banka, Emannuel Okwi na kisha mpira kumfikia Uhuru Selemani, ambaye hata hivyo ‘kishuti mtoto’ alichopiga kilidakwa kirahisi na kipa wa Yanga, Mghana, Berko.

Beki anayepanda kusaidia mashambulizi wa Yanga, Shadrack Nsajigwa, alimgeuza uchochoro beki wa kushoto, Juma Jabu na katika dakika ya 25 alimchomoka mlinzi huyo katika shambulizi ambalo hata hivyo liliishia mikononi kwa kipa wa Simba, Ali Mustapha ‘Barthez’, ambaye aliruka kuugombea mpira wa mwisho na Asamoah ambaye waligongana naye.

Kiungo Athuman Idd ‘Chuji’ aliinyima Yanga nafasi ya kupata goli wakati alipopiga shuti dhaifu na kushindwa kumalizia kazi ya gonga safi iliyofanywa baina ya Nsa Job, Nurdin Bakari hadi mpira kumfikia Chuji.

Kipa wa Simba, Barthez, alifanya kazi ya ziada kupangua shuti la Nsa Job katika dakika ya 72, baada ya kiungo huyo kupokea pasi safi kutoka kwa Jerry Tegete.

Patrick Ochan, aliyeingia uwanjani dakika 11 kabla ya mechi kumalizika kuchukua nafasi ya Mgosi, alileta ‘presha’ langoni mwa Yanga baada ya kumtengea pasi nzuri Uhuru Seleman, ambaye hata hivyo, alishindwa kufanya kilichotarajiwa baada ya shuti lake kuishia mikononi mwa kipa Berko.

Dakika moja baadaye beki wa kati wa Yanga, Nadir Haroub Cannavaro, alilimwa kadi ya njano kwa kumchezea rafu Shija Mkina aliyekuwa akielekea langoni mwa Yanga, hata hivyo mpira wa ‘fri-kiki’ uliopigwa na Okwi ulidakwa na Berko.

Fred Mbuna alikabididhiwa Ngao ya Jamii kutoka kwa Rais wa TFF, Leodgar Tenga na viongozi wa kampuni ya Vodacom iliyodhamini mchezo huo na

Kocha mwenye furaha wa Yanga, Mserbia Kostadin Papic, alisema baada ya mechi kuwa ni faraja kupata ushindi katika mechi hiyo yenye ushindani lakini hakuridhishwa na kiwango baada ya kufanya maandalizi makubwa.

Mzambia Phiri wa Simba alisema wachezaji wake walicheza vizuri lakini umaliziaji ulikuwa ni mbovu.

Vikosi vilikuwa; Simba: Ali Mustapha ‘Barthez’, Haruna Shamte, Juma Jabu, Juma Nyoso, Joseph Owino, Jerry Santo/Amri Kiemba (dk.47), Nicco Nyagawa/Shija Mkina (dk. 61), Mohammed Banka, Mussa Hssan ‘Mgosi’/Patrick Ochan (dk.79), Emannuel Okwi na Uhuru Selemani.

Yanga: Yaw Berko, Shadrack Nsajigwa ‘Fuso’/ Fred Mbuna (dk.74), Stephano Mwasika, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Isack Boakye, Ernest Boakye, Nurdin Bakari, Athiman Idd ‘Chuji’/ Godfrey Bonny (dk.59), Kenneth Asamoah/Jerry Tegete (dk.46), Nsa Job na Abdi Kassim ‘Babi’/Yahya Tumbo (dk. 77).

Enhanced by Zemanta

Posted under:  All Articles

Tags:  

Comments