Matuta yaipa Yanga Ngao ya Hisani

MIKWAJU ya penalti 3-1 imeipa Yanga Ngao ya Hisani ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na kuwapa furaha maelfu ya mashabiki wake waliofurika jana kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Hata hivyo, haikuwa kazi rahisi kuweza kupata ushindi huo baada ya timu hizo hasa Simba iliyoanza mchezo huo kwa kasi  na kutawala dakika 10 za mwanzo.
Baada ya hapo, timu hizo zilionyesha mchezo mzuri hasa viungo ingawa wakati mwingine mchezo ulionyesha kuwa wa kukamiana zaidi baada ya kumaliza dakika 45 za kwanza zikiwa suluhu 0-0.
Hali hiyo iliendelea hadi dakika 90 za mchezo huo. Katika upigaji wa mikwaju ya penalti, walioibuka mashujaa kwa Yanga ni Godfrey Bonny, Stephen na Isaac Boakye aliyecheza awali chini ya kiwango akimaliza kibarua huku penalti ya Ernest Boakye ikiokolewa na kipa Ali Mustafa wa Simba kuicheza.
Kwa upande wa Simba, wachezaji wake,  Emmanuel Okwi, Uhuru Suleiman na Amri Kihemba walishuhudia mikwaju yao ikipanguliwa na kipa Yaw Berko au kutoka nje huku Mohammed Banka pekee akifunga penalti yake.
Awali, kiungo mgeni Ernest Boakye, raia wa Ghana alijitahidi kwa kiasi kikubwa kuunganisha timu yake ya Yanga huku kazi kama hiyo ikifanya na Mohammed Banka wa Simba ambaye alikuwa akitoa pasi ndefu kwa washambuliaji wake.
Kwa muda mrefu kipindi cha kwanza, Simba walituliza mpira chini tofauti na Yanga ambao wamecheza zaidi mipira ya juu
Hali hiyo ilizifanya timu hizo  kushambuliana kwa zamu  huku zikiwategemea Kenneth Asamoah, Nsa Job kwa upande wa Yanga na Mussa Hassan ‘Mgosi’, Emmanuel Okwi na Uhuru Suleiman kwa Simba, safu za timu hizo hasa makipa Yaw Berko na Ali Mustafa wakiwa macho kuondosha hatari zote.
Asamoah, tofauti na mategemeo ya wengi alishindwa kutamba na kuonyesha makeke yake kutokana na kuwa majeruhi. Kocha Kostadin Papic alimpumzisha kipindi cha pili na nafasi yake kuchukuliwa na Jerry Tegete.
Katika mchezo huo, viungo wazoefu Abdi Kassim na Athuman Idd ‘Chuji’ walipotea kabisa mchezoni, pengine kutokana na kutochezeshwa nafasi zao za kawaida.
Katika mchezo huo wa jana, Chuji alicheza namba 8 huku Kassim  akicheza kama winga wa kushoto.
Kocha Papic aliwapumzisha Chuji, Kassim na Shadrack Nsajigwa na kuwaingiza Godfrey Bonny, Yahaya Tumbo na Fred Mbuna
Vikosi jana vilipangwa:
Simba:
Ali Mustafa, Haruna Shamte, Juma Jabu, Juma Nyosso,Joseph Owino, Jerry Santo, Nico Nyagawa, Mohammed Banka, Emmanuel Okwi, Uhuru Suleiman, Mussa Hassan ‘Mgosi’.
Yanga:
Yaw Berko, Shadrack Nsajigwa, Stephano Mwasika, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Isaack Boakye, Ernest Boakye, Nurdin Bakari, Athuman Idd, Kenneth Asamoah, Nsa Job, Abdi Kassim.

Enhanced by Zemanta

Posted under:  All Articles

Tags:  

Comments