Nyota Twiga Stars walilia posho

BAADA ya kurejea kutoka katika ziara yao nchini Marekani ikiwa ni moja ya maandalizi yao ya kujiandaa na fainali za Mataifa ya Afrika kwa wanawake hapo baadaye,wachezaji wa Twiga Stars wamelalamika kuhusu kulipwa posho zao na kudai hawajawahi kulipwa tangu waingie kambini kusaka kufuzu fainali hizo hadi sasa na hawafahamu hatma yao.

Wachezaji hao ambao waliwasili juzi jioni waligoma kuondoka katika ofisi za Shirikisho la Soka nchini (TFF) kwa madai ya kutolipwa fedha zao tangu waingie kambini hivyo kufanya mgomo wa kutoondoka kurejea makwao.

Hata hivyo, mgomo huo haukuzaa matunda baada ya kupewa majibu ya kutoridhisha na Mkurugezi wa Ufundi, Sunday Kayuni.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti huku wakitaka majina yao kutowekwa hadharani baadhi ya wachezaji hao walisema hawajawahi kupewa posho zao tangu waanze kambi huku kila siku wakiahidiwa kupewa na hadi sasa hawafahamu nini hatma yao baada ya kurejea katika ziara hiyo na kupewa majibu yasiyoeleweka.

“Inashangaza sana sisi kama wachezaji wa timu ya taifa hatuthaminiwi.. ebu fikiria tangu tuingie kambini wakati tukianza kuwania kufuzu fainali hizi mpaka sasa hakuna pesa yoyote tuliyopewa kila siku tunapewa ahadi sizizotekelezwa..tuliambiwa tutapewa baada ya kumaliza ziara yetu lakini tumefika hakuna wa kutusikiliza na wamekuwa wakitukwepa mara wanadai mpaka ligi kuu ianze ndio watatupa,”alisema mmoja wa wachezaji hao.

Katika hatua nyingine, msemaji wa Shirikisho la Soka (TFF), Florian Kaijage alisema ni kweli wamepokea malalamiko hayo kutoka kwa wachezaji hao na kudai hawajatumia busara katika kudai kwani waliwapa taarifa kwa sasa kuwa fedha zote za TFF zimezuiliwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ili zifanyiwe ukaguzi hivyo wavute subira kwa muda.

“Nashangaa kwa nini wameshindwa kuwa wavumilivu sisi tuliwapa taarifa wasubiri kutokana na TRA kutaka kukagua mapato yote ya TFF, lakini wameonekana kushindwa kutuelewa ila kikubwa tunachotaka wawe na subira mpaka hapo zoezi hili litakapomalizika halafu tutawaita na kumalizana nao sisi hatuna tatizo lolote na tutahakikisha kila kitu kinakaa sawa kwani tunatambua mchango wao kama wachezaji wa timu ya taifa,”alisema Kaijage.

Twiga Stars iko katika maandalizi ya mwisho ya kujiandaa na fainali za Mataifa ya Afrika kwa wanawake zitakazofanyika nchini Afrika kusini mapema mwezi Novemba baaba ya kufanikiwa kufuzu.

Enhanced by Zemanta

Posted under:  All Articles

Tags:  

Comments