Poulsen ataka `gonga` kama za Barcelona leo

Kocha Jan Poulsen wa Taifa Stars.
Kocha Jan Poulsen ameitaka Taifa Stars icheze pasi nyingi leo katika mechi yao ya kirafiki ya kimataifa dhidi ya Kenya wakati atakapoiongoza timu hiyo ya taifa ya Tanzania kwa mara ya kwanza tangu achukue madaraka ya kuifundisha kutoka kwa kocha Mbrazili, Marcio Maximo, aliyemaliza muda wake.
Mdenmark huyo amesema atatumia mfumo wa 4-3-3 katika mechi ya leo dhidi ya Wakenya hao ambao wametua na nyota wanaocheza Ulaya kama McDonald Mariga wa mabingwa wa Ulaya, Inter Milan, na Denis Oliech wa Auxerre ya Ufaransa. Mabingwa wa mwaka jana wa Ulaya, Barcelona, wanaotisha kwa soka la kuvutia la pasi nyingi, wamekuwa wakitumia mfumo wa 4-3-3.
Akizungumza jana, Poulsen alisema kuwa Stars ikiwa chini yake imefanya mazoezi kwa muda wa siku saba ambazo hazitoshi kuibadilisha timu katika kiwango anachokihitaji ingawa amewaandaa kucheza pasi nyingi kwa kutumia mfumo wa 4-3-3.
Poulsen alisema kuwa katika mchezo wa leo ambao atafurahi kuona timu yake inashinda, anataka kuangalia uwezo wa kila mchezaji ili kujua kikosi chake cha kwanza kwa sababu hajapata nafasi ya kuwaona wachezaji wote hasa wanaocheza nje ya nchi.
Alisema atawaanzisha katika kikosi cha kwanza nyota wote wa Stars wanaocheza soka la kulipwa nje ya nchi. Wachezaji wa Stars, Henry Joseph anayecheza soka Norway, Danny Mrwanda anayecheza Vietnam na Idrissa Rajab wa Sofapaka ya Kenya wamewasili na wameshiriki mazoezi ya jana ambayo hakuna shabiki aliyeruhusiwa kuingia kwenye Uwanja wa Karume, jijini Dar es Salaam, wakati Nizar Khalfan anayechezea Vancouver WhiteCaps ya Canada hatokuja.
“Kwa hakika ninahitaji kushinda katika mechi ya kesho (leo) ambayo ni wa kwanza kwangu, ninatarajia kufanya mabadiliko kadhaa katika mchezo huo ili nione uwezo wa kila mchezaji, hii ndio nafasi yangu ya kwanza,” alisema Poulsen.
Aliongeza ili Tanzania ifanikiwe, ni lazima nguvu zielekezwe katika soka la vijana.
Naye Kocha Mkuu wa Harambee Stars, Twahir Muhiddin, alisema kuwa anatarajia kuwa mchezo huo utakuwa na ushindani kwa sababu kila timu itatumia mechi hiyo kama sehemu ya maandalizi yake ya kuelekea katika fainali za Mataifa ya Afrika.
Muhiddin alisema kuwa licha ya kikosi chake kufanya mazoezi mara mbili, anaamini uzoefu wa wachezaji wao wa kulipwa na chipukizi utasaidia kuibuka na ushindi.
Alisema pia anaiheshimu Stars kutokana na wachezaji wake kuwa na uzoefu na hasa hivi karibuni kupata nafasi ya kucheza na moja ya vigogo vya soka duniani, timu ya Brazil.
“Kila timu itatumia mchezo huo kujifunza, sisi pia tunakabiliwa na mechi dhidi ya Guinea Bissau ugenini, kikubwa ni kujiamini,” aliongeza kocha huyo anayetaka makocha wazalendo wapewe heshima na kipaumbele katika timu za taifa.
Nahodha wa Harambee Stars, Julius Owino, ambaye hakuwa na maneno mengi, alisema “mechi ya leo ni ya kirafiki… atakayeshinda atakuwa na bahati.”
Viingilio vya mechi hiyo itakayofanyika kwenye Uwanja wa Uhuru, ni kati ya Sh. 3,000 na 20,000.
Mara ya mwisho Watanzania kukutana na Harambee Stars ilikuwa ni mwaka juzi katika mechi ya nusu fainali ya Kombe la Chalenji kwenye Uwanja wa Namboole jijini Kampala, Uganda ambapo timu ya Tanzania Bara, Kilimanjaro Stars, ililala kwa goli 1-0.
Enhanced by Zemanta

Posted under:  All Articles

Tags:  

Comments