Poulsen aanza vizuri

KOCHA wa Taifa Stas, Jan Poulsen ameanza kibarua chake cha kuinoa timu hiyo kwa sare ya bao 1-1 dhidi ya Harambee Stars ya Kenya katika mchezo wa kimataifa wa kirafiki uliofanyika kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.

Katika mchezo huo, Harambee Stars walikuwa wa kwanza kuandika bao katika dakika ya 13 baada ya Macdonald Mariga kupiga mpira wa adhabu ndogo na kumtungua kipa Shaaban Kado.

Faulo iliyofanywa na mabeki wa Stars, Shadrack Nsajigwa na Kelvin Yondani kwa mshambuliaji mwingine wa Kenya anayecheza soka ya kulipwa Ufaransa, Dennis Oliech ilimpa nafasi Mariga kuipa bao Harambee.

Hadi mapumziko, Harambee ambayo inanolewa na mzawa Twahir Muhiddin ilikuwa ikiongoza kwa bao hilo.

Lakini, Stars  waliweza kusawazisha  bao hilo dakika ya 57 ya mchezo  kupitia kwa Mrisho Ngassa baada ya kuitoroka safu ya ulinzi ya Harambee Stars.

Katika mchezo huo, Mariga na Oliech walibanwa sana  hasa kipindi cha pili huku Stars wakitawala mchezo huo kwa sehemu kubwa.

Kocha Poulsen alisema baada ya mchezo kuwa wachezaji wake hawakutulia hasa kipindi cha kwanza kiasi cha kushindwa kuwazuia wapinzani wao.

Alisema walijipanga vizuri kipindi cha pili kiasi cha kuwabana nyota wa Harambee wanaocheza soka ya kulipwa barani Ulaya na hata kupata bao la kusawazisha.

“Bado nataka kujenga  timu na kikubwa zaidi nilikuwa naangalia mchezo na kiwango cha kila mchezaji wangu kwani bado sijapata kikosi changu cha  kwanza,” alieleza kocha huyo.

Kocha Muhiddin aliisifu Stars  kwa kiwango chake lakini alisema Marcio Maximo hakuwa na fomesheni kama ambayo imeanza kuonekana kwenye mchezo wa jana huku Stars  ikicheza zaidi kama kitimu.

Alishauri Stars iwe na damu mchanganyiko badala ya kutegemea zaidi vijana kama ambavyo imekuwa ikifanya katika mechi zake zilizopita.

Naye Mariga aliieleza Stars kuwa inaonyesha kuwa soka ya Tanzania imepiga hatua ingawa inahitaji muda kuweza kufikia maendeleo ya Ulaya ambako kuna vifaa na zana nyingi zinazowezesha wachezaji kucheza vizuri zaidi.

Stars ambayo imekuwa kambini inajiandaa kuanza michuano ya Afrika kwa mechi ya ugenini mwezi ujao dhidi ya Algeria kusaka tiketi ya fainali za mwaka 2012.

Vikosi vilipangwa:

Stars: Shaaban Kado, Shadrack Nsajigwa, Idrissa Rajab/ Steven Mwasika, Kelvin Yondani/Aggrey Morris, Nadir Haroub, Nurdin Bakari, Jabir Aziz/ Athuman Idd, Abdi Kassim/ Abdulhalim Humoud, Mrisho Ngassa, Jerson Tegete/ Mussa Hassan, Uhuru Seleman/ Seleman Kassim.

Harambee:

Wilson Obungu, Julius Owino, George Owino, Lloyd Wahome, Edgar  Ochieng, Patrick Mzee, Macdonald Mariga, George Odhiambo, Dennis Oliech, John Barasa, Kevin Omondi

Posted under:  All Articles

Tags:  

Comments