Taifa stars kuvaana na Harambee stars

Photo of soccer player, Nizar Khalfan. Wilson ...
Image via Wikipedia

Jan Poulsen ataanza kibarua chake ramsi leo wakati Taifa Stars itapokuwa ikiwakabili Harambee Stars ya Kenya katika mchezo utakaochezwa kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.
Poulsen alichukua mikoba ya Mbrazil Marcio Maximo aliyemaliza mkataba wake mwezi Julai, huku Watanzania wengi wakiamini ataweza kuwaondoa katika nafasi ya 112, Stars inayoshika kwenye viwango vya soka vya fifa kwa sasa.

Akizungumzia mechi hiyo kocha wa Stars, Mdenmark, Poulsen amesema kuwa timu yake iko vizuri na wanategemea kutoa upinzani wa kutosha na wanatarajia ushindi katika mechi ya leo.

“Wachezaji wangu wako vizuri na wanaonyesha kila hali ya ushindi kwani wamekuwa makini kwa kipindi chote cha maandalizi na wote wameahidi kucheza kufa au kupona kuhakikisha wanashinda mechi hiyo.”

Alisisitiza kuwa japo ni mechi ya kirafiki, lakini watahakikisha wanapata ushindi ukizingatia ni mechi yake ya kwanza tangu alipopewa jukumu la kuifundisha timu hiyo na hivyo angefurahi kuona anapata ushindi wa kwanza akiwa na timu hiyo.

“Hii ni mechi yangu ya kwanza tangu nikabidhiwe kikosi hiki hivyo natamani na nitakuwa na furaha sana kama nitashinda mechi hii kwani itainua ari kwa wachezaji katika kujiandaa na michuano ya kimataifa ya Afrika,” alisisitiza Poulsen.

Katika mechi ya leo Poulsen amepanga kuwatumia wachezaji wengine watatu wanaocheza soka ya kulipwa  Danny Mrwanda, Henry Joseph na Nizar Khalfan.

Lakini zipo taarifa kwamba kiungo wa Vancouver Whitecaps, Nizar Khalfan hatoweza kufika kwa ajili ya mechi hiyo.

Kocha Poulsen alisema kuwa wachezaji ambao wameingia ni Idrissa Rajabu anayechezea Sofapaka ya Kenya, Henry Joseph, Norway na Danny Mrwanda Vetnam.

Kocha huyo alisema kuwa wachezaji wawili ambao ni Henry na Danny walitarajiwa kuwasili jana usiku kwa ajili ya mechi hiyo, lakini hawakuwa na taarifa kamili za mchezaji Nizar kurejea nchini kwa ajili ya mechi hiyo.

Kwa upande wa Idrissa yeye alikuwa ameshawasili siku mbili zilizopita kwa ajili ya mechi hiyo ya kirafiki kabla ya kukutana na Algeria katika mechi ya kuwania kufuzu kwa fainali za mataifa ya Afrika itakayofanyika Septemba 4.

“Kikosi changu kina wachezaji wengi chipukizi ambao wanahitaji kujifunza kutoka kwa wale wenye uzoefu hivyo naimani kwa kufanya hivi itakuwa changamoto kwao kujifunza baadhi ya vitu ambavyo wao hawana na kuwa wachezaji wazuri hapo baadaye”, alisisitiza Mdenmark huyo.

Katika mechi ya leo Taifa Stars itamkosa kipa wake Juma Kaseja ambaye ameumia mkono na  mshambuliaji Kigi Makasi anayesumbuliwa na tumbo.
Nahodha wa Stars, Shadrack Nsajigwa amesema hawatawaangusha Watanzania kwa kuhakikisha wanashinda mchezo huo.

”Tumejiandaa vizuri na nafikiri tutafanya vizuri , hatutawaangusha Watanzania wala mwalimu katika mchezo huu,”alisema Nsajigwa.

Mshambuliaji Mussa Hassan ‘Mgosi’ alisema hii ni nafasi nzuri kwao na anaamini watafanya kile kinachotarajiwa na Watanzania wengi.

Naye  Kocha mkuu wa Harambee Stars, Twahir Mohamed amesema kuwa mchezo wao wa leo dhidi ya Taifa Stars ni muhimu kwao kwani utawawezesha kujiandaa vyema kabla ya kucheza na timu ya Guinea Bissau.

“Mechi ya leo ni kipimo kizuri kwetu kwani itatuwezesha kujua mapungufu yetu katika kujiandaa na mechi za kimataifa ambapo moja ya mechi hizo ni dhidi ya Guinea Bissau,” alisema kocha huyo.

Harambee Stars waliowasili nchini  juzi wakiwa na mastaa wake wote mshambuliaji Denis Oliech wa Auxerre ya Ufaransa na Mc Donald Mariga anayeichezea Inter Milan ya Italia  jana walikuwa wakifanya mazoezi ya pamoja kwenye Uwanja wa Karume jijini Dar es Salaam.

Hata hivyo wachezaji wa Kenya wakiongozwa na Oliech waliiambia Mwananchi wamejiandaa vizuri na wataonyesha kiwango cha juu.

”Tumejiandaa vizuri na tutaonyesha kiwango cha juu kuona tunacheza mchezo mzuri ambao kila mmoja ataufurahia na tutashinda,”alisema Oliech.

Naye nahodha wa kikosi hicho Julius Owino alisema wataonyesha ushirikiano kwa kuwa Tanzania na wao wana ushirikiano mkubwa.
”Mpira utakuwa wa ushindani na tutaonyesha kiwango cha juu tukicheza kwa ushirikiano.

Katika hatua nyingine Oliech ametoa angalizo kwa wachezaji wa Tanzania kuwa kucheza nje sio rahisi kama watu wanavyofikiri na  unahitajika kujituma zaidi.

”Mimi nafikiri Watanzania wanapenda wenyewe kucheza nyumbani,  nafasi zipo ila inahitaji kujituma zaidi,”alisema Oliech.

Enhanced by Zemanta

Posted under:  All Articles

Tags:  

Comments