Kambi ya Ngumi shida, aibu

 IKIWA imebaki takribani miezi miwili kabla ya kuanza kwa Michezo ya Jumuiya ya Madola, timu ya taifa ya ngumi nchini imekuwa ikifanya mazoezi kwenye mazingira duni pamoja na kukosa daktari. Mashindano hayo yamepangwa kuanza kutimua vumbi Oktoba 3 mjini New Delhi, India na yatashirikisha wanamichezo kutoka nchi 72 za jumuiya hiyo. Mwananchi ilishuhudia mazoezi ya mabondia hao yanayofanyika kwenye Uwanja wa Ndani wa Taifa chini ya Kocha Premier Hurtado ambayo yalikuwa na upungufu mwingi ukiwamo wa vifaa vya mazoezi. Mabondia hao walilazimika kusubiriana katika mazoezi ya kujenga misuli kutokana na uhaba wa ‘punching bags’ kuwa mbili tu huku mabondia hao wakiwa 16. Mbali na punching bags, pia vikinga ulimi vimeendelea kuwa tatizo kwao kwani vifaa hivyo ni kumi ambavyo havitoshelezi idadi ya mabondia 16. Mwananchi ilizungumza na nahodha wa timu hiyo, Joseph Martin, na kusema kuwa, “Uhaba wa vifaa ni tatizo kubwa sana kwenye timu yetu. “Huwa inatulazimu mabondia wanne kutumia punching bag moja na baadhi ya vifaa huwa tunabadilishana, hatuna daktari wa timu na ikitokea bondia ameumia kama ni mfanyakazi, basi ataenda kutibiwa kazini kwake. “Lakini, kuna wale ambao si wafanyakazi huwa na wakati mgumu wanapoumia kwani hawana pa kukimbilia, pamoja na kukosa daktari pia dawa na maji ni tatizo kubwa,” alisema Martin. Kocha Hurtado alisema , “Tazizo vifaa natoka nyumbani mapema ili kuwai mazoezi, lakini hali inakuwa tofauti vifaa ni shida pia.” Mmoja wa viongozi wa shirikisho la mchezo huo ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini alisema kuwa, “Ni kweli tunao upungufu wa vifaa kwani vile tulivyokuwa navyo awali vimekwisha, tunashindwa kununua kutokana na ukata unaotukabili.” “Hatupati ruzuku yoyote kutoka Shirikisho la Ngumi la kimataifa (AIBA) hadi 2011 ndiyo tutaanza kupokea misaada toka kwao kwani tumerejeshewa uanachama hivi karibuni, pia hatuna mfadhili hata mmoja ingawa mabondia wetu wamestahimili yote. “Tunahangaika kila siku kutafuta wafadhili naamini akijitokeza hata mmoja timu yetu itafika mbali kimataifa,” alisema kiongozi huyo.
Enhanced by Zemanta

Posted under:  All Articles

Tags:  

Comments