Mkwasa: Kipigo 6-0 Twiga Stars kimetufunza

Kocha mkuu wa timu ya taifa ya soka ya wanawake, Twiga Stars, Boniface Mkwasa, amesema kuwa licha ya timu yake kupokea kichapo cha 6-0 kutoka kwa wenzao wa Afrika Kusini, Banyana Banyana, timu hiyo imefaidika kiufundi na mechi hiyo ya kirafiki ya kimataifa.

Mkwasa amesema kuwa makosa waliyoyafanya wachezaji wake katika mechi hiyo, yamemsaidia kufahamu mapungufu waliyonayo na sasa ataelekeza nguvu katika kuyafanyia kazi ili kuimarisha kikosi hicho kabla ya muda wa fainali za Mataifa ya Afrika kwa wanawake haujafika.

Mkwasa alisema kuwa anaamini baada ya kuyafanyia kazi mapungufu aliyoyaona, pamoja na kambi watakayoenda kuweka nchini Marekani, wachezaji wake watakuwa wamepata uzoefu wa kutosha na wataenda katika fainali hizo nchini Afrika Kusini wakiwa wameiva.

Alisema kuwa atafurahi kuona Twiga Stars inapata mechi nyingine ya kirafiki ya kimataifa na timu ngumu ili kupata uzoefu wa kukabiliana na ‘vigogo’.

Twiga Stars imefuzu kucheza fainali hizo kwa mara ya kwanza baada ya kuzifunga timu za Ethiopia na Eritrea na ushindi wa magoli 8-1, ambao iliupata dhidi ya Eritrea hapa nyumbani ndio uliwavutia Banyana Banyana na kuwaalika.

CHANZO: NIPASHE

Posted under:  All Articles

Tags:  

Comments