Simba wampa Phiri siku 7

Uongozi wa Klabu ya Simba umempa siku saba kocha wao mkuu, Mzambia Patrick Phiri, kuungana na timu hiyo na endapo atashindwa kufanya hivyo, atakuwa amevunja mwenyewe mkataba wa kuifundisha timu yao.

Phiri ambaye ana rekodi nzuri akiwa na Simba, aliondoka nchini na kwenda kwao Zambia kwa mapumziko baada ya kikosi chake kurejea nchini kikitokea jijini Kigali, Rwanda, walikokuwa wakishiriki michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati ‘Kombe la Kagame’.

Hata hivyo, mara kadhaa Phiri amedaiwa kuisumbua klabu hiyo kila mara anapokwenda kwao na kuilazimu timu kufanya maandalizi ikiwa na makocha wasaidizi.

Akizungumza na Nipashe jana, mmoja wa viongozi wa juu wa Simba, alisema kuwa wamemuandikia barua kocha huyo juzi na kumtaka awe amerejea katika muda waliompa ili aiandae timu vyema kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara.

Kiongozi huyo alisema kuwa wamefikia hatua hiyo baada ya kuchoshwa na dalili za utoro wa Phiri, licha ya kuridhishwa na uwezo mkubwa alio nao na pia kufahamu mazingira ya timu pinzani watakazokutana nazo katika ligi.

“Tumemueleza kwamba anatakiwa aheshimu mkataba ambao amesaini mwenyewe. Kutokana na hali hii, tunaweza kusitisha mkataba wake,” alisema kiongozi huyo.

Makamu Mwenyekiti wa klabu hiyo, Godfrey Nyange ‘Kaburu’, alisema ni kweli wamempa siku saba Phiri na endapo atashindwa kurejea mapema, watatafuta kocha mwingine kwani kutokuwepo kwake kunaharibu program za klabu, na hasa kwa kujua kuwa amekuwa akichelewa kila mara anapopata ruhusa ya kwenda kwao.

“Kwa upande wa wachezaji tuko vizuri, kocha ndiye anayetuchelewesha,” alisema Makamu Mwenyekiti huyo ambaye pia anaongoza kamati ya usajili.

Phiri aliyejiunga kwa mara ya kwanza na klabu hiyo mwaka 2005, msimu uliopita alifanikiwa kuweka rekodi ya kuipa ubingwa Simba huku ikiwa imeshinda mechi 20 kati ya 22 na kutopoteza hata mechi moja.

Hata hivyo, imeelezwa kuwa kuchelewa kwa Phiri kumewastua viongozi wa Simba na tayari wameanza mazungumzo na makocha wengine kadhaa, akiwemo Sylersaid Mziray.

CHANZO: NIPASHE

Posted under:  All Articles

Tags:  

Comments