Tanzania yapanda chati netiboli

Tanzania imepanda chati za dunia katika mchezo wa netiboli baada ya timu ya taifa kuonyesha kiwango kizuri wakati wa mashindano ya kirafiki yaliyofanyika Uingereza hivi karibuni.Kwa mujibu wa taarifa iliotolewa na chama cha netiboli, CHANETA, Tanzania imekwea kutoka nafasi ya 22 mpaka ya 20.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa kwa upande wa wa Afrika Tanzania bado inashika nafasi ya nne, na kwamba kwa sasa CHANETA inaanza kutafuta nafasi ya kushiriki michuano ya dunia.

“Tumepanda kwa kiasi kikubwa sana,” ilisema taarifa hiyo ya wiki hii.

Taarifa ya CHANETA imesema kutokana na kupanda chati huko, chama hicho kinayaomba makampuni mbali mbali pamoja na wadau wa mchezo huo kutoa michango yao ili Tanzania iweze kushiriki michuano mbali mbali na kupanda chati zaidi.

Taarifa ilisema moja ya mashindano ambayo yanaweza kuipandisha chati Tanzania na kufuzu kushiriki michuano ya dunia ni ambayo itafanyika Afrika Kusini Septemba 5-12 mwaka huu.

“Tunaanza kampeni za kutafuta nafasi ya kushiriki michuano ya dunia ya netiboli kuanzia Septemba tano,” ilisema taarifa.

Hii itakuwa mara ya pili kwa Tanzania kupanda chati ya dunia katika mchezo wa netiboli tangu kuingia kwa uongozi mpya CHANETA baada ya kuwa haishiriki michuano yoyote kwa kipindi kirefu cha uongozi uliopita.

Posted under:  All Articles

Tags:  

Comments