Jan Poulsen amrithi Maximo Taifa Stars

Kamati ya uteandaji ya Shirikisho la soka Tanzania (TFF), jana ilitangaza rasmi kwamba kocha wa zamani wa timu ya taifa ya Denmark, Jan Poulsen, (64), ameteuliwa kuwa kocha mpya wa timu ya taifa, Taifa Stars.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa TFF, Fredrick Mwakalebela, alisema kocha huyo ataanza rasmi kazi ya kuinoa Stars Agosti moja na ameteuliwa na kamati hiyo baada ya kupokea mapendekezo yaliyotolewa na Kamati ya Ufundi ya TFF.

Mwakalebela alisema kuwa mbali na kuwa kocha mkuu, Poulsen ambaye aliifikisha timu ya taifa ya vijana ya Denmark katika hatua ya fainali za FIFA za umri chini ya miaka 20 mwaka 2007, pia ni mkufunzi wa makocha anayetambuliwa na FIFA.

Mwakalebela alisema kwamba Poulsen amepata nafasi hiyo baada ya kuwazidi makocha wengine nane waliobakia katika mchujo wa mwisho.

“Makocha 59 waliomba kazi hii kutoka nchi mbalimbali, lakini mchakato ulipoanza, tulibakiwa na makocha 26 na uliendelea tena na kubakia 10, lakini kabla ya kuendelea na mchakato huo, wawili walituandikia barua kwamba wameshapata kazi sehemu nyingine na hivyo tuliwaita nane waliobaki na kuwahoji na hatimaye tumepata kocha mpya,” alieleza Mwakalebela bila kutaja majina ya makocha hao waliofika hatua hiyo ya mwisho ya mchujo.

Alisema kuwa kocha huyo ataingia mkataba wa kuifundisha Stars kwa muda wa miaka miwili na tayari ameshakubali jukumu hilo baada ya kujulishwa kwamba yeye ndiye aliyeshinda.

Uteuzi huo umefanyika kwa kuhusisha wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF iliyokutana juzi jijini Dar es Salaam wakati mchakato wa kumpata mrithi huyo wa Mbrazil Marcio Maximo anayemaliza mdua wake, ulianza kufanyika Februari mwaka huu.

TFF iliendesha mchakato huo kutokana na kutomuongezea Maximo mkataba kwa awamu ya tatu baada ya kuifundisha Stars tangu mwaka 2006.

Kocha mpya wa Stars atakutana na jukumu la kuhakikisha kwamba Tanzania inafuzu fainali zijazo za Kombe la Mataifa ya Afrika na mechi yake ya kwanza itakuwa Septemba 4, ugenini dhidi ya Algeria.

Katika kipindi cha miaka minne ambayo Maximo ameifundisha Stars, alifanikisha timu hiyo kucheza fainali zilizopita za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ligi za ndani (CHAN), ambazo zilifanyika mwaka jana nchini Ivory Coast.

CHANZO: NIPASHE

Posted under:  All Articles

Tags:  

Comments