Viingilio Stars, Brazili vyalalamikiwa

Kiungo Abdulhalim Homoud `Gaucho` (jirani na kamera) akijifua kwenye Uwanja wa Karume, pamoja na wachezaji wenzake wa timu ya taifa, Taifa Stars, inayojiandaa na mechi ya kirafiki dhidi ya timu ya taifa ya Brazili itakayofanyika Jumatatu Juni 7, kwenye Uwanja wa Taifa, Jijini Dar es Salaam. (Picha: Omar Fungo)

Siku moja tu baada ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kutangaza viingilio vya mechi ya Jumatatu ya kimataifa ya kirafiki kati ya Taifa Stars na Brazili, wadau kadhaa wa soka wamelalamika ni kudai vya juu mno kulinganisha na hali halisi ya kiuchumi waliyo nayo mashabiki wengi wa soka nchini.

Wakizungumza na Nipashe kwa nyakati tofauti jana, wadau hao wa soka walisema wameshangazwa na viingilio hivyo vya kuanzia cha Sh. 30,000 hadi Sh. 200,000, wakidai kwamba vinawabagua mashabiki maskini wanaojazana kila siku viwanjani ili kuziunga mkono timu za nyumbani na badala yake, (viingilio hivyo) vimewajali watu wenye pesa pekee.

Wadau hao wameelezea vilevile kushangazwa na viingilio hivyo kuwa juu, ilhali Serikali ilishawahi kutangaza kuwa imetenga Sh. Bilioni 7 kwa ajili ya kuzileta timu mbalimbali zinazoshiriki Kombe la Dunia ili zije nchini kabla ya michuano kuanza nchini Afrika Kusini na kuitangaza Tanzania.

“Zile Bilioni 7 za kodi yetu alizotangaza Mwenyekiti wa Kamati ya Rais ya Kombe la Dunia (Dk. Shukuru Kawambwa) ziko wapi? Hatupingi kuchangia, lakini Serikali lazima ijue kwamba mashabiki wengi wa soka nchini ni Watanzania na si Wamarekani wala Wasweden… kwa mwenendo huu wa kutubagua maskini katika mechi kama hizi, wajue kwamba siku moja watabaki na uwanja usio na faida, tutashindwa kwenda kabisa viwanjani,” alisema shabiki mmoja wa soka jijini Dar.

“Wao walisema zipo fedha za kuleta timu kama hii ili ziwe sehemu ya kutangaza utalii wetu… sasa iweje tena wanatugeuzia kibao kwa kutaka tuchangie kwa gharama kubwa kiasi hiki? Watakosea sana kama wanataka gharama zinazoingiwa na Serikali kwa mechi za maonyesho ziwe zikilipwa moja kwa moja na wananchi kwa staili hii. Madhara yake baadaye ni makubwa, hasa pale maskini watakaposusa mechi kama hizo na kuridhika na michuano ya kuwania mbuzi mitaani,” aliongeza shabiki mwingine.

Maoni ya baadhi ya wadau wengine maarufu kuhusiana na viingilio vya mechi hiyo vya Sh. 30,000, Sh. 50,000, Sh. 80,000, Sh. 100,000, Sh. 150,000 na Sh. 200,000 kwa tiketi zilizokwishauzwa za VIP yalikuwa kama ifuatavyo:

Yussuf Nguya – Mchezaji Manyema Rangers/ Lindi

Mchezaji huyu alisema kwamba tangazo la viingilio lililotolewa juzi na TFF limefuta ndoto yake ya kutaka kuishuhudia ‘live’ Brazili na kujifunza kutoka kwa wanasoka wa timu hiyo waliojaa vipaji

“Binafsi, nilikuwa natamani sana kuangalia mechi hii. Lakini, nasikitika kusema kwamba itaniwia vigumu kwenda uwanjani siku hiyo. Ni mechi inayotaka watazamaji wenye vipato vya juu, mimi si mmoja wao. Kiingilio cha chini cha Sh. 30,000 ni cha juu mno kwangu,” alisema Nguya.

Kenny Mwaisabula – Kocha

Kocha huyu maarufu na aliyepitia klabu kadhaa za Ligi Kuu nchini wahi alisema amesikitishwa mno na viingilio vilivyotajwa, kwani haviwapi vijana wengi maskini nchini kupata fursa ya kujifunza kwa kuona moja kwa moja kutoka kwa wachezaji wakubwa wa Brazili.

Alisema TFF walipaswa kuweka viingilio vikubwa zaidi kwa viti vya madaraja ya juu kama VIP na kupanga kiingilio cha walau Sh. 10,000 kwa mashabiki wa chini ambao siku zote hujaza viwanja na pia kuwapa fursa wachezaji yosso kumudu kwenda uwanjani siku hiyo.

“Viingilio hivi vinasikitisha… naamini vimewatenga vijana wetu wengi wanaotaka kujifunza kupitia mechi hii,” alisema Mwaisabula.

Iddi Pazi – Kipa wa zamani Stars/Kocha

Kipa huyu namba moja wa zamani Pilsner, Simba na Taifa Stars, alisema ameshangazwa na hadi sasa ni kama haamini juu ya viingilio vya juu mno vilivyotangazwa na TFF kwa mechi ya Stars na Brazili.

“Kwanza huu mchezo una faida gani kwetu? Ungeanza mchezo huu halafu ukafuatia wa mashindano (CHAN) unaotukabili dhidi ya Rwanda, tungesema ni sehemu ya maandalizi yetu. Lakini huu hauko hivyo… nimesikitishwa mno na viingilio hivi,” alisema Pazi.

Iddi Azzan – Mbunge wa Kinondoni (CCM)

Mbunge huyu wa Jimbo la Kinondoni kupitia chama tawala, na ambaye ni mdau mkubwa wa soka, alisema haoni tatizo kuhusiana na viingilio vilivyopangwa.

“Kweli viingilio ni vikubwa na havijawai kutokea nchini. Lakini lazima tuelewe kuwa siku hizi mpira ni gharama, hata kwa nchi za Ulaya, mchezo kama huu viingilio vyake huwa ni vya juu,” alisema Azzan.

Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ – Kocha wa Ilala

Kocha huyu aliyewahi kuzifundisha Kajumulo, Simba na timu kadhaa nchini kabla juzi kuipeleka Ilala nusu fainali ya Kombe la Taifa, alisema kwa upande wake, anaamini viingilio vilivyotangazwa havina tatizo.

Alisema hiyo ni njia mojawapo ya kupunguza fujo na vitendo vya kihuni katika siku hiyo.

“Mie nakwambia, wakiweka viingilio vya chini watakaribisha hasara… watasogeza fujo mlangoni. Watanzania wanapaswa kubadilika, wenzetu wamepiga hatua na siku hizi hata tiketi za bure hazitolewi,” alisema Julio.

Desemba 31 mwaka jana, Serikali ilitangaza kuwa imetenga Sh. Bilioni 7 kwa ajili ya kuzihamasisha nchi zinazoshiriki fainali Za Kombe la Dunia (KAMA Brazili) kuja nchini na hatimaye kupitia mpango huo, Tanzania ijitangaze duniani kote.

Mwenyekiti wa Kamati ya Rais ya FIFA 2010, Dk. Shukuru Kawambwa, aliwaambia waandishi wa habari kuwa pesa hizo zilizotengwa na Serikali, zitatumika kwa mambo mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kuzigharamia timu zitakazoletwa.

CHANZO: NIPASHE

Posted under:  All Articles

Tags:  

Comments