Taifa Queens warejea vichwa chini

Mchezaji wa Timu ya taifa ya netiboli, Taifa Queen akifunga.

Timu ya taifa ya netiboli, Taifa Queens, imerejea juzi ikitokea nchini Uingereza ambako ilienda kwa ajili ya kucheza mechi za kirafiki na nchi za huko.

Kikosi hicho ambacho kiliondoka na wachezaji tisa, kimeshindwa kufanya vizuri kutokana na kuwa na majeruhi wengi.

Akizungumza mara baada ya kikosi hicho kuwasili, mratibu wa safari hiyo, Joel Mwakitalu, alisema kuwa wamejitahidi lakini tatizo la majeruhi liliwaathiri sana.

“Tumeshindwa kufanya vizuri kutokana na kukabiliwa na majeruhi,” alisema Mwakitalu.

Aliongeza kuwa pamoja na kushindwa kurejea na kombe lakini wamejifunza mengi ikiwemo kupata uzoefu wa kucheza na timu ambazo zinashiriki michuano mikubwa ya netiboli duniani.

Alisema pia kuwa wachezaji wamefurahia ziara hiyo, ambayo imewajenga kisaikolojia.

Naye kocha wa timu hiyo, Mary Protasi, alisema kuwa somo walilopata wachezaji wake katika mechi hizo ni kubwa na litawasaidia sana watakapokutana na timu nyingine katika michezo ijayo. Timu iliondoka nchini wiki mbili zilizopita.

CHANZO: NIPASHE

Posted under:  All Articles

Tags:  

Comments