Talib aitwa Simba awang`oe Waarabu

Kocha mkuu wa klabu ya Simba `Wekundu wa Msimbazi`, Mzambia, Patrick Phiri.

Katika kuhakikisha kwamba Simba inasonga mbele katika michuano ya Kombe la Shirikisho, uongozi wa klabu hiyo umemuongeza katika benchi la ufundi kocha na mchezaji wake wa zamani, Talib Hilal.

Talib atashirikiana na kocha mkuu wa klabu hiyo ya ‘Wekundu wa Msimbazi’, Mzambia, Patrick Phiri, lengo likiwa ni kuhakikisha kwamba mabingwa hao wapya wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara wanaiondoa Haras El Hadood ya Misri katika michuano hiyo ya kimataifa na hatimaye wanatinga hatua ya nane bora.

Talib ambaye sasa anaishi Oman, aliwahi kushirikiana na kocha Mkenya, James Siang’a mwaka 2003 katika mashindano ya Klabu Bingwa Afrika na kuivua ubingwa wa mashindano hayo klabu ya Zamalek ya Misri, ambayo ni kubwa na maarufu zaidi nchini humo kuliko wapinzani wa sasa, El Hadoud.

Akizungumza na Nipashe jana, mmoja wa viongozi wa juu wa Simba, alisema kuwa mazungumzo na Talib yalishafanyika mapema na tayari mchezaji wao huyo wa zamani amekubali kushirikiana na Phiri katika kuiimarisha Simba.

Kiongozi huyo alisema pia kwamba, Simba itakwenda kuweka kambi Oman kabla ya kuelekea Misri ili kurejeana na wapinzani wao na wakiwa huko (Oman), watacheza mechi mbili za kirafiki.

“Tumeona ni vyema kujiimarisha katika kila idara, Talib anafaa katika hatua hii kwa sababu anazifahamu vyema timu za waarabu na pia tumekubali ushauri wake wa kuipeleka timu yetu kwenda kujifua huko kwani tutapata nafasi ya kutumia vifaa vua kisasa vya michezo wakati wa maandalizi,” aliongeza kiongozi huyo.

Aliongeza kwamba kabla ya kuondoka, Simba wanatarajia kufanya harambee ili kupata fedha za kutosha katika maandalizi yao ambayo pia yanahusisha mashindano ya Kombe la Kagame.

Katika mechi ya kwanza ya raundi ya pili dhidi ya El Hadood iliyochezwa juzi kwenye uwanja wa Taifa, Simba iliibuka na ushindi wa magoli 2-1 kupitia kwa wachezaji wake Mussa Hassan ‘Mgosi’ na Mganda, Emmanuel Okwi.

Mechi ya marudiano itafanyika kati ya Mei 7 na 9 na Simba inahitaji sare ya aina yoyote ili isonge mbele katika mashindano hayo yanayoandaliwa na Shirikisho la Soka la Afrika (CAF).

Wakati huohuo, mechi ya kwanza ya Simba na El Hadood iliyochezwa juzi kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam imeingiza zaidi ya Sh. Milioni 106.

Taarifa ambazo Nipashe ilizipata jana, zimedai kuwa

mechi hiyo iliyohudhuriwa na mashabiki wengi lakini walioshindwa kuujaza Uwanja wa Taifa unaochukua watazamaji walioketi 60,000, iliingiza mapato mengi zaidi katika eneo la VIP B..

Kiingilio cha chini katika mechi hiyo kilikuwa ni Sh. 5,000 wakati cha juu kilikuwa Sh. 30,000.

Baada ya mechi, El Hadood waliondoka nchini jana alfajiri na kurejea kwao Misri, tayari kwa maandalizi ya mechi yao ya marudiano.

Simba ambayo ilifikia hatua ya sasa baada ya kuwashindilia Lengthens ya Zimbabwe kwa jumla ya magoli 5-1, inahitaji sare ya aina yoyote dhidi ya El Hadood ili kusonga mbele katika michuano hiyo.

CHANZO: NIPASHE

Posted under:  All Articles

Tags:  

Comments