Mechi Simba, Yanga yasogezwa mbele

Simba
Yanga

Mechi ya marudiano ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara kati ya Simba na Yanga imesogezwa mbele hadi Aprili 18 na sasa itafanyika kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam imefahamika.

Awali, mechi hiyo ilipangwa kufanyika kesho, ambapo Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) pamoja na klabu hizo mbili, ziliafikiana mchezo huo ufanyike kwenye Uwanja wa Uhuru.

Akizungumza jana, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo, Serth Kamuhanda, alisema kwamba serikali na wadau hao watatu wamekubaliana mechi hiyo ifanyike kwenye uwanja huo mpya kwa ajili ya kudhibiti usalama wa mashabiki na kulinda amani.

Kamuhanda ambaye aliongoza kikao cha siku mbili kilichoanza juzi, alisema kwamba wote kwa pamoja walikubaliana kwamba endapo mchezo huo ungefanyika kwenye Uwanja wa Uhuru, usalama ungekuwa ni mdogo na vile vile hauwezi kukidhi matakwa ya watazamaji ambao wanatarajiwa kuwa ni wengi, huku akiongeza kwamba uwanja huo bado unafanyiwa matengenezo ya kuuboresha.

Hata hivyo, Kamuhanda alishindwa kuweka wazi ni kiasi gani cha mgao wa mapato ambacho klabu hizo zitapata baada ya kukubali kuhamisha mchezo huo uliokuwa unasubiriwa kwa hamu na mashabiki wa soka hapa nchini.

“Tumeshazungumza na tunaendelea kuzungumza, tunaendelea kulifanyia kazi suala hilo,” alisema kwa kifupi katibu huyo wa wizara.

Mwenyekiti wa Simba, Hassan Dalali, alisema kwamba maamuzi hayo waliyofikia ni sahihi na yamefanyika kwa kila upande kuridhia mabadiliko hayo.

Dalali alisema kwamba wanawataka mashabiki wake kuwa na subira na wanawaomba radhi kwa usumbufu uliojitokeza juu ya mabadiliko yaliyofanywa.

Naye Mwenyekiti wa Yanga, Imani Madega, alisema kuwa wameridhika na maamuzi yaliyofikiwa katika kikao hicho na yanatokana na sababu kuu mbili za msingi.

Madega aliitaja sababu ya kwanza ni ya kiusalama na nyingine ni ya kuelekea katika kupata ufumbuzi wa kilio chao cha mapato pale wanapocheza kwenye uwanja huo.

“Sasa haki itatendeka, walichofanya ni jambo la kuendeleza soka na hiyo itasaidia kuufanya mchezo huo uchezwe bila ya malalamiko,” alisema Madega.

Aliongeza kwamba hadi kufikia jana ni wazi kwamba kilio chao kimesikika na matumaini yanaonekana baada ya kufanyika kwa mazungumzo hayo.

Kutokana na mabadiliko hayo, Katibu mkuu wa TFF, Fredrick Mwakalebela, alitangaza viingilio vya mchezo huo kuwa ni Sh. 40,000 kwa eneo la VIP A, Sh. 30,000 VIP, Sh. 20,000 VIP C wakati eneo la rangi ya machungwa mzunguko ni Sh. 15,000.

Mwakalebela alisema kuwa eneo la viti vya rangi ya machungwa nyuma ya magoli ni Sh. 10,000, viti vya bluu Sh. 7,000 na viti vya kijani tiketi zitauzwa kwa gharama ya Sh. 5,000.

Alisema kuwa mechi zote za funga dimba za ligi hiyo zilizopangwa kufanyika Aprili 17 sasa zitachezwa Aprili 21.

Simba na Yanga waligomea kutumia uwanja huo mpya kutokana na makato ya asilimia 40 yanayokwenda kwa wamiliki wa uwanja huo na maandalizi ya mchezo na kuona jambo hilo kuwa ni sawa na kuwanyonya wakati wao ndio wanaoingia gharama katika kuandaa timu.

CHANZO: NIPASHE

Posted under:  All Articles

Tags:  

Comments