Phiri arejea, Lengthens waja Alhamisi

Kocha mkuu wa Simba, Patrick Phiri

Wapinzani wa Simba katika mashindano ya kuwania ubingwa wa Kombe la Shirikisho, timu ya Lengthens kutoka Harare, Zimbabwe wanatarajia kutua nchini Alhamisi tayari kuwakabili wenyeji wao Jumapili kwenye Uwanja wa Uhuru.

Akizungumza na gazeti hili jijini Dar es Salaam jana, Msemaji wa Simba, Clifford Ndimbo, alisema kuwa msafara wa timu hiyo unaofadhiliwa na ofisi ya Rais wa nchi yao, Robert Mugabe, unatarajiwa kuwa na wachezaji 22 pamoja na viongozi watano.

Ndimbo alisema kwamba maandalizi ya kuwapokea wageni hao yamekamilika na wanatarajia kwamba watawaweka katika hoteli nzuri kama ambavyo uongozi wa timu hiyo uliwafanyia wachezaji wao walipokuwa Harare.

Alisema kwamba wameamua kuja mapema ili kuzoea hali ya hewa ya Dar es Salaam ili waweze kupata matokeo mazuri katika mechi hiyo ya marudiano.

“Tumejipanga vizuri juu ya mchezo huo wa marudiano, tunataka mambo yaende vizuri na hatimaye tusonge mbele, kila kitu kimekamilika kwa hatua kubwa,” alisema Ndimbo.

Wakati huo huo, Kocha mkuu wa Simba, Patrick Phiri na kiungo, Emmanuel Okwi, walirejea nchini jana na kuelekea Zanzibar kwa ajili ya kuanza kambi kujiandaa na mchezo huo.

Phiri aliyekuwa kwao Zambia kwa mapumziko alifika nchini saa saba mchana na Okwi, aliyekwenda kwao Uganda kusalimia, naye aliwasili saa sita mchana na wote wawili walipanda ndege kuwafuata wenzao walioondoka saa sita mchana kwa usafiri wa boti kwenda kambini Zanzibar.

Katika hatua nyingine, kipa chaguo la kwanza la timu hiyo, Juma Kaseja, anatarajiwa kurejea nchini leo akitokea India ambako alikwenda kupiga picha za matangazo ya biashara na kampuni moja ya watu binafsi.

Simba inahitaji sare ya aina yoyote ili kusonga mbele kwenye mashindano hayo ambapo mshindi atakutana na timu kati ya Banks ya Ethiopia au Haras Al Hadoud ya Misri.

CHANZO: NIPASHE

Posted under:  All Articles

Tags:  

Comments