Tanzania hakuna mawakala wa soka-Mgosi

MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Tanzania na klabu ya Simba, Mussa Hassan Mgosi amesema tatizo kubwa kwa wachezaji wa Tanzania kucheza soka ya kulipwa ni mawakala.

Kwa muda sasa,wachezaji wengi wa Tanzania wamekuwa wakitamani kucheza soka ya kulipwa Ulaya na sehemu nyingine duniani, lakini wameshindwa kufanikiwa kwa kukosa mawakala wa uhakika wa kutafutia timu wachezaji.

“Mawakala wetu wao hawana uhusiano wa moja kwa moja na klabu za sehemu mbalimbali badala yake wamekuwa wakiongea na mawakala wengine ili kuwahunganishia kwa timu hivyo inakuwa vigumu kidogo kwetu kupenya,” alieleza Mgosi

Aliongeza Mgosi kuwa hata hivyo idadi ya mawakala walioko Tanzania ni wachache sana kwa hiyo inakuwa vigumu kwao kumchukua kila mchezaji na kwenda kumtafutia timu ya kufanya majaribio.

Kinara huyo wa ufungaji wa Simba msimu huu alisema yeye bado ana nia ya kucheza soka nje ya nchi sehemu yoyote ile iwe Uganda, Kenya, Ulaya hata DR Congo.

“Kwa sasa kikubwa kwangu ni fedha endapo nitapata timu sehemu yoyote ambayo itanilipa vizuri nipo tayari kwenda nahitaji kukuawa kikosa zaidi, lakini tatizo ndio hilo la mawakala.”

“Siku hizi soka mtu anacheza sehemu yoyote kwa kuangalia maslahi yako, mpira ndio maisha yangu nahitaji kupata fedha zaidi kwa sasa nilikiwa na nguvu zangu,” alisema Mgosi mshambuliaji huyo mfupi na mwenye kasi.

Mgosi ambaye alikuwa hapa na timu kwa mechi ya Kombe la Shirikisho la Soka Afrika (CAF) hakusita kuonyesha hisia zake katika mchezo ujao wa timu ya Taifa, Taifa Stars dhidi ya Somalia unaotarajiwa kuchezwa Machi 27 jijini Dar es Salaam kuwania kufuzu kwa fainali za CHAN 2011 nchini Sudan.

“Nadhani maandalizi yetu safari hii si mazuri ukilinganisha na mwaka juzi tulipofuzu, japokuwa tuna nafasi kubwa ya kushinda mechi yetu ijayo dhidi ya Somalia.

“Ndio wachezaji wote tulioteuliwa tupo kwenye klabu na wote tunafanya vizuri, lakini nadhani tulihitaji kukaa kambini muda mrefu zaidi kujiandaa na michezo hii kuliko ilivyo kwa sasa.”

Aliongeza kwa hali zetu zilivyo hawana budi kuwa na utamaduni wa kukaa kambini muda mrefu kidogo ili kutujingea kujiamini.

“Jambo lingine ambalo ningependa kuwaomba Watanzania ni kujifunza kukubali matokeo yote ya uwanjani kushinda, kushindwa na sare.

“Mashabiki wa Tanzania matokeo wanachojua wao ni kuishinda tu hakuna kingine timu ikifungwa kila mtu anawashutumu utadhani kwamba sisi tunapenda kufungwa,” alilalama Mgosi.

“Ukiangalia nchi za wenzetu mashabiki watashangilia timu yao hata kama imefungwa jambo hilo linatia moyo sana kwa mchezaji kujua kuna watu wanakuthamini.”

Posted under:  All Articles

Tags:  

Comments