Simba Bingwa 2010

Wachezaji wa Simba wakimbeba juu kocha wao Mzambia Patrick Phiri baada ya kuwaongoza kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara kwenye Uwanja wa Uhuru, jijini Dar es Salaam baada ya mechi yao dhidi ya Azam FA jana. Simba ilishinda 2-0. (Picha: Tryphone Mweji)

Mkenya Mike Barasa alikuwa shujaa jana wakati magoli yake mawili yapoisaidia timu yake ya Simba kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara kufuatia ushindi wa 2-0 dhidi ya Azam FC katika mechi iliyofanyika kwenye Uwanja wa Uhuru Jjijini Dar es Salaam.

Barasa, aliyejiunga na Simba katika usajili wa dirisha dogo la usajili Novemba mwaka jana akitokea kwa mahasimu Yanga baada ya kukataa kuongeza mkataba wake uliokuwa umemalizika, alikuwa nyota mkubwa katika mechi ya jana.

Aliipa Simba bao la kwanza katika dakika ya 8 tu tangu mchezo kuanza akimalizia kazi nzuri iliyofanywa na Mganda Hillary Echesa na akaongeza la pili katika dakika ya 62.

Simba walitawala mchezo na goli hilo la mapema liliashiria njaa waliyokuwa nayo wana Msimbazi katika kutwaa ubingwa huo walioukosa kwa misimu miwili mfululizo iliyopita ambayo ilitawaliwa na mahasimu wao Yanga.

Mussa Hassan ‘Mgosi’ alipoteza nafasi ya kuipa Simba goli la pili, wakati aliposhindwa kuuwahi mpira wa pasi ya Ulimboka Mwakingwe akiwa karibu na kipa wa Azam katika dakika ya 10.

Barasa alikosa nafasi nyingine ya kufunga katika dakika ya 32 kufuatia krosi ya Mgosi na Azam wakajibu kwa shambulizi kali dakika tano baadaye lakini shuti la John Bocco liliishia kwenye mikono salama ya Juma Kaseja.

Kipindi cha pili kilianza kwa Azam kuwatoa Wagaluka katika dakika ya 46 na nafasi yake kuchukuliwa na Selemani Kassim na Said Sued, ambaye nafasi yake ilijazwa na Ally Manzi.

Mike Barasa tena, aliwanyanyua vitini mashabiki kibao wa Simba waliofurika uwanja mzima wakiwa wamevalia mavazi ya rangi nyekundu na nyeupe, baada ya kufunga goli la pili akiiwahi pasi ya mchezaji aliyetokea benchi Uhuru Selemani katika dakika ya 62.

Filimbi ya mwisho ilizua shamrashamra kubwa za mashabiki wa Simba walioingia barabarani katika mitaa mbalimbali ya jiji, huku magari ya watu binafsi na madaladala yakipeperusha bendera za rangi nyekundu nyeupe, kuashiria ushindi huo mkubwa zaidi kwa ngazi ya klabu nchini Tanzania.

Ubingwa huo unamaanisha kwamba Wekundu wa Msimbazi wataiwakilisha nchi katika michuano ya Ligi ya Klabu Bingwa mwakani, ambao wenzao Yanga mwaka huu wametolewa mapema mno baada ya kufungwa mechi zao zote mbili za kwanza dhidi ya Saint Eloi Lupopo ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo.

Polisi walilazimika kuweka ulinzi nyumbani kwa mtabiri maarufu nchini Sheikh Yahaya, kufuatia hofu ya mashabiki kuvamia, kufuatia kauli yake ya mapema kwamba Simba haitatwaa ubingwa msimu huu licha ya kuongoza kwa takriban msimu mzima.

Mtabiri huyo alipohojiwa alisikika akisema kupitia kituo kimoja cha radio jana kuwa yeye anachotabiri ni baina ya Simba na Yanga na sio Simba na Azam, akidai klabu hizo mbili za mwisho ni watoto wa baba mmoja.

Uwanjani mashabiki wa Simba walibeba bango kubwa lililosomeka: ”SIMBA BINGWA LAZIMA, SHEKH YAHYA SI MUNGU” katika kupinga utabiri wa mnajimu huyo.

Timu zilikuwa; Simba: Juma Kaseja, Haruna Shamte, Juma Jabu, Juma Nyosso, Kelvin Yondani, Mohammed Banka, Hillary Echesa, Ramadhan Chombo ‘Redondo’, Mussa Hassan ‘Mgosi’, Mike Barasa/ Mohammed Kijuso (dk.78), Ulimboka Mwakingwe/Uhuru Selemani (dk. 55).

Azam: Vladimir Niyonkuru, Ibrahim Shikanda, Malika Ndaule/Mau Bofu (dk.65), Tumba Sued, Salum Sued, Himid Mao, Danny Wagaluka/Selemani Kassim (dk. 46), Salum Abukar, John Bocco, Shaban Kisiga, Said Sued/ Ally Manzi (dk. 46).

CHANZO: NIPASHE

Posted under:  All Articles

Tags:  

Comments