Arsenal hapatoshi leo..

ARSENAL inaikaribisha FC Porto mchezo wa marudiano wa 16 bora Ligi ya Mabingwa Ulaya kwenye Uwanja wa Emirates jijini London ikiwa na jukumu gumu zaidi.

Timu hiyo ambayo ilifungwa mabao 2-1 mjini Oporto mwezi uliopita licha ya kuwa na asilimia 50-50 ya kumchezesha nahodha wake, Cesc Fabregas aliyeumia Jumamosi akiikabili Burnley inatakiwa kutimiza mambo mawili muhimu.

Vijana hao wa Arsene Wenger wanatakiwa leo kuishambulia Porto kwa muda wote wa dakika 90 za mchezo, wakati huo huo kuizuia timu hiyo ya Ureno isipate bao.

Porto, ni timu ambayo inafahamika kwa mchezo wake wa kushambulia kwa kushtukiza, ikiwatumia zaidi wachezaji wake wenye vipaji, ingawa inakutana na Arsenal ambayo imekuwa haifungiki kwenye mechi za Ulaya, isipokuwa mwaka jana ilipofungwa na Manchester United kwenye nusu fainali.

Gazeti la Record la Ureno linaeleza kuwa Porto inajivunia wachezaji wake, Radamel Falcao, Silvestre Varela, Givanildo Vieira de Souza au Hulk na Ruben Micael kuweza kuisumbua Arsenal katika mchezo wa leo.

Falcao, mwenye umri wa miaka 24, raia wa Colombia anajivunia mabao manne ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu.

Mchezaji huyo amekuwa akilinganishwa na Carlos Tevez wa Manchester City, raia wa Argentina.

Lakini, Arsenal itaweza kumzuia raia huyo wa Colombia kwa kumchezesha Sol Campbell na Thomas Vermaelen kama mabeki wa kati wakiwa na jukumu la kumchunga Falcao ambaye hana nguvu, mfupi.

Lakini, Vermaelen, beki anayeongoza kwa kufunga mabao Ligi Kuu England anatakiwa kuzuia mipira kutoka sehemu ya kiungo ya Porto ili kumnyima nafasi ya kuchezea mpira na kupata mabao.

Kwa upande wa Hulk, mwenye miaka 23, raia wa Brazil, amefunga mabao matatu. Ni mshambuliaji aliye kamili anayejivunia nguvu na mmaliziaji mzuri.

Lakini, licha ya kucheza wakati mwingine kama winga, ni mchoyo anayependa kucheza kila mpira unaomfikia

Katika mchezo wa leo, Arsenal itaweza kumzuia kwa kushambulia zaidi na kumzuia kusonga mbele huku beki Gael Clichy akiwa na jukumu la kumkaba.

Lakini, kocha Arsene Wenger anaweza kuwatumia viungo Samir Nasri na Thomas Rosicky kutimiza jukumu hilo, ingawa Andrei Arshavin pia ni mshambuliaji anayeweza kumfunika Hulk.

Mchezaji mwingine ambaye Arsenal haina budi kumchunga ni Varela, akiwa na umri wa miaka 25, raia huyo wa Ureno ambaye alifunga bao la kwanza dhidi ya Arsenal katika mchezo uliopita akifanikishwa na David Silva wa Valencia ya Hispania ni mwepesi, mwenye mashuti makali na krosi hatari anapocheza upande wa kulia au kushoto.

Katika mc hezo huo, Arsenal itamzuia kwa kumchunga iwe ni Gael Clichy au Bacary Sagna asiingie eneo la hatari.

Yeye ndiye huwalisha mipira Falcao au Hulk . Lakini, hataweza mchezo wa nguvu kama mabeki wa Arsenal wataaamua kutumia nguvu kumzuia.

Mchezaji mwingine ambaye Arsenal haina budi kuwa makini naye ni Ruben Micael, yeye ana miaka 23, raia wa Ureno ambaye hajafunga bao lolote Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Licha ya ugeni wake Porto, lakini ameonyesha uwezo mkubwa hasa akiwa eneo la hatari la timu pinzani licha ya kucheza kama kiungo.

Ili kumzuia, Arsenal inatakiwa kumtumia ama Alexandre Song, Denilson au Cesc Fabregas kama atacheza kumnyima nafasi ya kupata mpira na kuuchezea.

Mechi nyingine ya leo ni baina ya Fiorentina ya Italia dhidi ya Bayern Munich ya Ujerumani nchini Italia. Bayern ilishinda mabao 2-1 katika mchezo wa kwanza.

Comments