Yanga yaaga rasmi Afrika, Simba ikipasha

Timu ya Yanga.

Yanga jana iliaga rasmi Ligi ya Klabu Bingwa Afrika katika kihunzi cha kwanza tu baada ya kufungwa bao 1-0 na timu ya FC Lupopo jijini Lubumbashi, JK Kongo, habari kutoka huko zilisema.

Akizunguza na Nipashe Jumapili kwa njia ya simu, msemaji wa Yanga Louis Sendeu alisema bao la wenyeji lilifungwa na Yaliembe katika dakika ya 76 kuipa FC Lupopo ushindi wa jumla wa mabao 4-2 wa raundi ya kwanza. Ili kusonga mbele, Yanga ilihitaji kushinda angalau mabao 2-0 baada ya kufungwa 3-2 nyumbani wiki mbili zilizopita lakini mvua iliyonyesha mchana jana haikuweka mazingira mazuri ya kufanya hivyo.

Wachezaji wa Yanga walikuwa wakiteleza mara kwa mara kutokana na uwanja kuwa na matope, alisema Sendeu ambaye alieleza pia mchezo uliamuliwa kwa haki na waamuzi kutoka Cameroon.

Kocha mkuu wa Yanga Kostadin Papic aliridhishwa na kiwango cha timu yake baada ya mechi hiyo, alisema Sendeu lakini “akalalamika timu haikuwa na bahati.”

Yanga inarudi nyumbani kesho Jumatatu kuendelea na harakati za kutetea ubingwa wa ligi kuu ya Bara, alisema Sendeu.

Katika mchezo mwingine wa klabu Afrika, lakini wa kirafiki, Simba iliichapa Zesco ya Zambia kwa mabao 4-1 kwenye Uwanja wa Uhuru anaripoti Faustine Feliciane.

Mchezo huo ulichelewa kuanza kwa zaidi ya nusu saa baada ya waamuzi kutaka walipwe kwanza posho yao kabla ya kufanya kazi.

Bao la kwanza la Simba ambayo inajiandaa na mechi ya raundi ya pili ya Kombe la Shirikisho la klabu za Afrika Machi 13, lilifungwa na Mike Barasa katika dakika ya 37 kwa shuti la mbali kabla ya Nico Nyagawa kuipatia la pili dakika tatu kabla ya mapumziko mabeki wa Zesco walipodhani ameotea. Zesco inayojiandaa na ligi kuu ya Zambia itakayoanza katikati ya mwezi ujao ilikwenda mapumziko ikiwa bao moja nyuma baada ya Enock Sakala kufunga kutokana na pasi ya kichwa ya Cliford Chipwalo.

Bao la tatu la Simba lilifungwa na Barasa katika dakika ya 64 kwa penalti baada ya Mohammed Kijuso kuangushwa ndani ya eneo la hatari na akaongeza lingine dakika mbili baadaye kwa shuti la mbali.

Simba: Ally Mustafa, Haruna Shamte, Jabir Aziz, Anthony Matangalu, Joseph Owino, Paul Terry, Uhuru Selemani, Nico Nyagawa, Kelvin Chile, Mike Barasa na Abdallah Seseme.

CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

Posted under:  All Articles

Tags:  

Comments