Simba nguvu sawa na `Paka`

Mussa Hassan `Mgosi`.

Mussa Hassan ‘Mgosi’ jana aliwanyima Simba ushindi wa kwanza wa Kundi A la michuano ya Kombe la Tusker baada ya kukosa penati dhidi ya wageni Sofapaka katika mechi ambayo kocha wa mabingwa hao wa Kenya alidai kuwa refa Mzanzibari aliwabeba wenyeji.

Simba walipata penati hiyo katika dakika ya 44 iliyotolewa na refa Ramadhani Ibdada wa Zanzibar, baada ya kiungo Hillary Echessa kufanyiwa madhambi na beki wa Sofapaka Edgar Otieno ndani ya eneo la hatari, lakini shuti la Mgosi, liliishia mikononi mwa kipa wa Sofapaka Wilson Obungu ambaye alipangua penati hiyo.

Katika mechi iliyojaa ushindani, Simba ndio waliokuwa wa kwanza kufika langoni mwa Sofapaka wakati beki Juma Jabu alipopoteza nafasi ya kufunga katika dakika ya 4 ya mchezo baada ya kupiga nje mpira uliotokana na krosi safi ya beki wa kati Joseph Owino.

Wekundu waliendelea kuliandama lango la wageni na dakika tatu baadaye, walipoteza nafasi nyingine ya kufunga wakati mshambuliaji Ramadhani Chombo ‘Redondo’ alipopiga shuti lililoishia mikononi mwa kipa wa Sofapaka, Obungu.

Sofapaka waliokuwa wakicheza kwa kujihami wakiringia ushindi mnono wa 3-1 wa mechi yao ya kwanza dhidi ya Mtibwa katika siku ya ufunguzi, walinusurika tena katika dakika ya 38 wakati ‘Redondo’ tena alipochelewa kuifikia krosi ya Mussa Hassan Mgosi, na hivyo kumpa mwanya kipa wa Sofapaka kuzima hatari hiyo ya langoni mwake.

Simba walifanya mabdiliko katika dakika ya 55 kwa kumtoa Redondo na nafasi yake kuchukuliwa na yosso Uhuru Selemani, huku nyota wa zamani wa wapinzani wa jadi Yanga, Mkenya Mike Barasa, akiingia kuchukua nafasi ya Boban.

Mabingwa wa Kenya “walilibip” lango la Simba katika dakika ya 57 wakati mshambuliaji John Onami alipomtoka beki wa Simba Owino lakini kipa wa Msimbazi Juma Kaseja alikuwa mwepesi zaidi kuuwahi mpira kabla mshambuliaji huyo kupiga shuti.

Sofapaka walifanya mabadiliko katika dakika ya 58 kwa kumtoa John Onami na kumuingiza Anthony Kimani lakini Wakenya hao walijikuta wakibaki 10 uwanjani kufuatia beki wao Heskey Wanyama kutolewa kwa kadi ya pili ya njano kutokana na kuchelewesha mpira, wakati timu ikionekana kuhitaji sare zaidi ili kujihakikishia kucheza hatua ya nusu-fainali. Onami alikuwa na kadi ya njano ya kwanza tayari aliyoipata mapema.

Mgosi ambaye hakuwa na siku nzuri jana, aliinyima Simba goli kwa mara nyingine dakika sita kabla mechi kumalizika wakati alipopiga shuti dhaifu pembeni ya goli akiwa jirani mno na lango.

Baada ya mechi hiyo, kocha wa Simba Mzambia Patrick Phiri aliwasifu Sofapaka kuwa wana timu nzuri lakini wanaonekana tangu mwanzo kuwa walikwenda kutafurta sare, ambayo imewapeleka hatua ya nusu-fainali tayari kutokana na kuwa na pointi 4, ambazo zinaweza kufikiwa na Simba tu endapo itaifunga Mtibwa kesho.

“Tuta hakikisha tunashinda dhidi ya Mtibwa,” alisema Phiri, huku kocha wa Sofapaka Robert Matano akimtuhumu mwamuzi kuwa aliipendelea Simba.

Michuano hiyo inaendelea leo ambapo Yanga inaikabili Mafunzo ya Zanzibar katika mechi ya Kundi B.

Vikosi vilikuwa; Simba: Juma Kaseja, Salum Kannoni, Juma Jabu, Kelvin Yondani, Joseph Owino, Mohammed Banka, Nicco Nyagawa, Hillary Echessa, Mussa Hassan ‘Mgosi’, Haruna Moshi ‘ Boban’ na Ramadhani Chombo ‘Redondo’.

Sofapaka: Wilson Obungu, Heskey Wanyama, James Situma, Tumba Kilonzo, Edga Otieno, Nicolaus Muyuti, Kevin Ochieng, Humphrey Ochieng, Mugaliya Bob, Patrick Kagogo na John Onami.

CHANZO: NIPASHE

Posted under:  All Articles

Tags:  

Comments